Tanzania yapiga hatua uhuru wa vyombo vya habari

0

Na Grace Semfuko, MAELEZO

MKURUGENZI wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, amesema Tanzania imepiga maendeleo makubwa katika kulinda uhuru wa vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kufanya mageuzi ya kuboresha sheria za vyombo hivyo, ambazo zinaendana na viwango vya kimataifa.

Alisema, Serikali ya Tanzania inaendelea na dhamira yake ya kuendeleza mazingira huru, huku akivitaka vyombo hivyo kuhakikisha vinasambaza taarifa sahihi zenye uwiano kwa maslahi ya umma.

Makoba alisema hayo jijini Dar es Salaam, alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, katika Mkutano wa 14 wa Chama cha Mawasiliano Afrika Mashariki (EACA), ambapo pia alisema takwimu za kidunia zinaonesha Tanzania imefanya vizuri katika eneo hilo.

“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa Tanzania imepata maendeleo ya kupongezwa katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, kulingana na fahirisi ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ya 2024, taifa letu limepanda kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka 2024,” alisema Makoba.

Ameeleza kuwa, uboreshaji huo mkubwa si wa takwimu tu, bali unaakisi jitihada za makusudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo ina dhamira thabiti ya kuboresha mazingira ya vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru, haki, na bila hofu kama msingi wa maadili ya kidemokrasia ya Tanzania.

Aidha, alisema kutokana na kukua kwa vyombo vya habari vya kidijitali, kumekuwepo na changamoto ya kuenea kwa kasi kwa taarifa potofu, changamoto ambayo ameitaja kuwa ni ya kimataifa na kuvitaka vyombo vya habari vya Tanzania kudumisha ukweli na uadilifu

“Vyombo vya habari lazima viwe macho katika jukumu lake la kuhabarisha umma na kuandika habari za ukweli, uandishi wa habari wenye maadili lazima uwe mhimili wa vyombo vyetu vya habari, kuhakikisha kwamba uhuru wa vyombo vya habari hauathiriwi na harakati za kuibua hisia au kueneza uwongo,” alisisitiza Makoba.

Ameitaja mikakati ya Serikali kuwa ni pamoja na kuunga mkono vyombo vya habari kwa kuwa na utaratibu wa kuwezesha mazungumzo kati ya Serikali na wadau wa habari, ili kuhakikisha hoja zinazohusika zinaweza kushughulikiwa kwa njia ya kujenga na kwa ushirikiano.

Pia, ameeleza mikakati mingine ni kuwekeza katika mipango ya kujenga uwezo ili kuongeza ujuzi na weledi wa wanahabari na kuwawezesha kukidhi matakwa ya mandhari ya vyombo vya habari inayobadilika kwa kasi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here