Dodoma
SERIKALI ya Tanzania na Uingereza Aprili 8, 2025 zilikutana na kujadili kwa pamoja Taarifa ya Uchambuzi wa Kina iliyoonesha fursa za kuongeza thamani madini za muda Mfupi na wa Kati wa Madini Muhimu na Mkakati ya Tanzania ambayo iliwasilishwa na Ujumbe kutoka Mpango wa Manufacturing Afrika unaofadhiliwa na Uingereza.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde, ujumbe huo ukiongozwa na Mkuu wa Sehemu ya Diplomasia na Uchumi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini, Tamsin Clayton, ulibainisha fursa zipatazo 13 za kuongeza thamani madini ya aina zipatazo 11 za madini muhimu na mkakati yanayopatikana nchini.
Uchambuzi huo unalingana na moja ya mikakati inayoandaliwa na Wizara ya Madini ambayo inatoa fursa kwa Tanzania kuzalisha mapato ya hadi Dola za Marekani Bilioni 11 kwa mwaka huku ukitarajia pia kuzalisha ajira hususan kwa vijana na wanawake.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Mavunde aliushukuru ujumbe huo kwa mchango wao muhimu na kusisitiza kwamba taarifa hiyo iliyowasilishwa inakwenda sambamba na mkakati wa Serikali ambao Wizara imeundaa kwa ajili ya kuwezesha manufaa ya haraka ya uongezaji thamani madini nchini.
Alisisitiza kuhusu umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa madini ili kubaini kiwango cha madini muhimu na mkakati kilichopo nchini na kuongeza kwamba, shughuli za uongezaji thamani madini hayo kwa kiwango kikubwa kitategemea hali ya upatikanaji wa rasilimali hiyo.
Waziri pia alisisitiza haja ya kuwa na ushirikiano wa kitaifa, akitolea wito wa utekelezaji wa mpango wa Serikali kwa pamoja ili kufanikisha kuzitumia fursa hizo, akirejelea ahadi ya Wizara yake kuongeza ushirikiano na taasisi na mashirika muhimu ya Serikali.
Waziri Mavunde alitoa shukrani kwa timu yake ya kiufundi ya Wizara kwa kuwa karibu na kushiriki kikamilifu katika utafiti huo na kubainisha dhamira yake ya kuendeleza ajenda ya kuongeza thamani ya madini nchini Tanzania.