TANZANIA, UAE wakubaliana kuondoa suala la utozaji kodi mara mbili

0

Na Benny Mwaipaja, Dubai

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zimetia saini mkataba  wa makubaliano ya kuondoa utozaji Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi ya Mapato kati ya nchi hizo mbili, yaani Agreement on Avoidance of Double Taxation and Prevention of Fiscal Evasion on Income Taxes.

Mkataba huo umetiwa saini katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Umoja wa Falme za Kiarabu mjini Dubai na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mohamed Bin Hadi Al Hussain, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE)

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa kusainiwa kwa Mkataba huo ni jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozifanya Mwezi Februari, 2022 katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo aliagiza kuondolewa kwa changamoto hiyo ili kukuza mahusiano ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano katika masuala ya kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

“Ni matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu ku tutaona uwekezaji mkubwa ukikua kati ya nchi zetu hizi, hasa kutoka Uarabuni ambao wana mitaji mikubwa lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza, hata wawekezaji, wafanyabiashara wa Tanzania wataweza kufanya biashara bila kuwa na mashaka ya kutozwa kodi mara mbili hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili,” alisema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba alisema, UAE imeingia mikataba kama hiyo na nchi 139 duniani, zikiwemo nchi za Afrika Mashariki, lakini Tanzania ilikosa baadhi ya fursa za uwekezaji kutoka mataifa hayo ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa hizo zinazotokana na kuondolewa kwa changamoto hizo za utozaji kodi mara mbili.

“Hatua hii itavutia uwekezaji wa mitaji na ujenzi wa viwanda vitakavyosaidia kuchakata bidhaa zitakazozalisha ajira kwa vijana wa kitanzania na itachachua uchumi kwa kuongeza wigo wa kodi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazo uzwa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni,” alisema Dkt. Nchemba

Alisema, Tanzania imekaa kimkakati kutokana na kuwa lango la biashara kutokana na uwepo wa bahari, idadi kubwa ya watu, kuwa katika eneo la kimkakati kijiografia pamoja na kuwa na soko la uhakika katika eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 177.

Hivyo, kusainiwa kwa mkataba huo kutafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi  ambapo makampuni makubwa yanayomilikiwa na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu  yatakwenda kuwekeza nchini  Tanzania ambapo uwekezaji huo utaleta faida katika sekta za uzalishaji, ukuaji wa viwanda pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania. 

Pamoja na kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Waziri mwenzie wa Fedha wa upande wa Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo ukamilishwaji wa Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji yaani “Agreement on Promotion and Protection of Investment” ambapo walizielekeza timu za wataalam wa pande zote mbili kukutana na kuanza majadiliano ya mkataba huo kwa faida za pande zote.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru, alisema kuwa kusainiwa kwa Mkataba huo wenye vipengele 31 ambavyo nchi hizo mbili zimekubaliana kuvitekeleza, utawezesha mtu ama taasisi inayofanya biashara katika nchi hizo kutozwa kodi ya faida ya mapato upande mmoja badala ya utaratibu wa awali ambapo walikuwa wakitozwa kodi hiyo kila upande na kuzua malalamiko kutoka kwa wawekezaji.

“Baadhi ya watu wanaweza kutafsiri kuwa mikataba ya aina hii ni kusamehe kodi, lahasha, hii ni mikataba inayoweka kanuni ya kuzuia uhamishaji wa kodi kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa kuzingatia uwekezaji unatoka katika eneo gani, inahusisha kulinda mitaji ya wawekezaji wa nchi husika,” alisema Mafuru.

Alisema, kuwepo kwa mkataba huo kutawejengea wawekezaji uhakika na imani ya kuwekeza mitaji yao nchini, jambo ambalo halikuwepo huko nyuma, na kwa kuwa mikataba ya namna hiyo inalindwa Kimataifa, na kama kutakuwa na kutokuelewana kwa namna yoyote, mikataba hiyo itakuwa msingi wa majadiliano.

Maeneo yanayoguswa na makubaliano hayo ni utozaji wa kodi katika mapato yanayotokana na biashara, usafiri wa anga na majini, mali zisizohamishika, riba, gawio, uvunaji wa rasilimali za asili, wafanyakazi na watafiti, wanafunzi malipo ya pensheni na Hifadhi ya Jamii pamoja na masuala ya michezo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohamed Bin Had Al Hussain, alisema kuwa hatua iliyofikiwa ya kuondoa utozaji kodi ya mapato mara mbili kati ya Tanzania na UAE kutavutia wawekezaji wengi zaidi kutoka katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa pande hizo mbili.

Alipongeza jitihada zinazofanywa na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kufanikisha jambo hilo la kuondoa utozaji wa kodi ya mapato mara mbili na kwamba hatua hiyo itavutia mitaji na wawekezaji wengi kutoka nchi za Kiarabu kuja kuwekeza Tanzania na kuomba pia suala la kulinda mitaji na uwekezaji lifanyiwe kazi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here