Tanzania, Estonia kushirikiana Mapinduzi ya Kidigitali duniani

0

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA na Estonia zimekubaliana kushirikiana kufikia mapinduzi ya kidigitali duniani.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi wakati wa kikao maalumu nje ya Kongamano la Kumi la Utawala wa Masuala ya Mtandao lililofanyika kwa siku mbili katika Jiji la Tartu nchini Estonia hivi karibuni.

Kongamano hilo lilishirikisha zaidi ya watu 500 kutoka nchi 67 duniani, wengi wakiwa watoa maamuzi ya maendeleo ya mambo ya kidijitali duniani, watunga sera, waratibu wa utekelezaji sera na wadau wa maendeleo.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa pili kulia) akishiriki katika Kongamano la Mawaziri wa nchi mbalimbali zilizodhamiria kujenga uchumi imara wa kidigitali waliokutana jijini Tullin, Estonia hivi karibuni. Wengine walioshiriki ni Mariin Ratnik, Waziri mdogo wa Mambo ya Maendeleo na Uchumi wa Estonia, Margus Tsahkna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Olalunbosun Tijani, Waziri wa Mawasiliano Ubunifu na Uchumi wa Kidijitali wa Nigeria na Mercy Wanjau, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya. (Picha kwa hisani ya Tume ya TEHAMA).

Naibu Waziri Mahundi yeye na Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Nele Leosk ambaye ni Balozi wa Masuala ya Kidigitali wa nchi hiyo katika mkutano huo, kwa niaba ya nchi zao walizungumzia umuhimu wa kushirikiana katika uendelezaji na ukuaji wa akili mnemba, teknolojia ya mifumo kuzungumza na usalama wa mitandao.

Aidha, walizungumzia masuala ya namba ya utambulisho ya kidijitali, uhuru wa data, ukuzaji kampuni za ubunifu na uchumi wa kidigitali.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Nele Leosk ambaye ni Balozi wa Mambo ya Kidigitali wa Estonia wakati walipokutana hivi karibuni jijini Tartu, Estonia wakati wa Kongamano la Kumi la Utawala wa Mtandao ulioshirikisha zaidi ya nchi 67 duniani. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga na kulia ni Mali Liis Vahi, Kansela wa Idara ya Mambo ya Kidijitali na Diplomasia ya Kimtamdao. (Picha kwa hisani ya Tume ya TEHAMA).

Katika mkutano huo mbali ya Naibu Waziri, wawakilishi wengine wa Tanzania walikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga na Afisa Ubalozi wa Tanzania nchini Uswisi, Joyce Malipula. Kwa upande wa Estonia, alikuwepo pia Mali Liis Vahi, Kansela wa Idara ya Mambo ya Kidijitali na Diplomasia ya Kimtamdao.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Maryprisca alishiriki pia katika Kongamano la Mawaziri wa nchi mbalimbali waliodhamiria kujenga uchumi imara wa Kidigitali.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi (kulia) akiwa katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Nele Leosk ambaye ni Balozi wa Mambo ya Kidigitali wa Estonia wakati wa kikao maalumu kilichoazimia Tanzania na Estonia kuwa na ushirikiano katika masuala mbalimbali ya Kiteknolojia hivi karibuni jijini Tartu, Estonia. Kulia kwa Naibu Waziri Mahundi ni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga. (Picha kwa hisani ya Tume ya TEHAMA).

Katika mkutano huo Naibu Waziri Maryprisca asisitiza nia ya Tanzania kuusuka uchumi wa kigiditali kwa kuhakikisha inaimarisha mifumo ukiwemo wa taarifa binafsi kwa wananchi wa Tanzania.

Mbali ya Tanzania, mawaziri wengine walioshiriki ni Mariin Ratnik, Waziri mdogo wa Mambo ya Maendeleo na Uchumi wa Estonia, Margus Tsahkna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Estonia, Dkt. Olalunbosun Tijani, Waziri wa Mawasiliano Ubunifu na Uchumi wa Kidijitali wa Nigeria na Mercy Wanjau, Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kenya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here