TANAPA watakiwa kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii

0

Na Happiness Sam, Arusha

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeitaka TANAPA kuendelea kuboresha maeneo ya vivutio vya utalii ili kuvutia idadi kubwa ya wageni na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa.

Hayo yamezungumzwa lMachi 25, 2025, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustine Holle wakati wa ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na shughuli zinazotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

“Hifadhi hii ina vivutio vingi vya asili na tumeshuhudia maporomo ya maji pamoja na wanyama wa aina mbalimbali wakiwa katika maeneo yao ya asili hivyo ni jukumu letu kuhakikisha kuwa maeneo haya yanaboreshwa zaidi na kufikika kwa urahisi na wageni wote.”

Aidha, Holle aliongeza, “Tunahitaji pia kutoa fursa nyingi za uwekezaji kwa watu binafsi hususani wazawa ili kuongeza ubora wa huduma jambo litakalovutia wageni wengi kuitembelea hifadhi hii.”

Vilevile, Holle alisema kuwa kama Kamati wameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha ikiwemo ukarabati wa barabara na ujenzi wa nyumba za kisasa za kulala wageni, hatua hizi ni ishara ya maendeleo makubwa ambayo yatarahisisha kufikika kwa maeneo mengi na kuimarisha huduma ya malazi kwa wageni.

Akimwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Dkt.Robert Fumagwa ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, alitoa shukrani kwa Kamati hiyo kufika na kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha kwa lengo la kukagua pamoja na kuangalia shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Dkt. Fumagwa alisema “Ushauri wa Wajumbe wa Kamati umepokelewa na tutahakikisha mapendekezo hayo yanafanyiwa kazi na miradi hii inakamilika kwa wakati ili kuongeza ufanisi wa hifadhi na kuifanya kuwa kivutio bora kwa watalii wa ndani na nje ya Tanzania.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru – Amir Mohammed Mkalipa, alitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha, miradi ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Arumeru, huku ikichochea maendeleo pamoja na kuboresha maisha yao.

Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga, ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, alisema kuwa TANAPA itaendelea kuisimamia miradi yote inayojengwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha na kuhakikisha inakidhi viwango vilivyokusudiwa sanjari na kushirikiana na vijiji vinavyozunguka hifadhi ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa hifadhi hiyo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imefanya ziara ya kukagua miradi miwili ya maendeleo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha. Miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa barabara yenye urefu wa Kilomita 16, ambayo imegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 419, pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa za kulala wageni ambazo gharama yake ni Shilingi Milioni 204.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here