MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Mkilia amesema, taarifa binafsi za kila Mtanzania zinatakiwa kulindwa ili kuepuka madhara ambayo mtu anaweza kuyapata iwapo zitawekwa hadharani.
Dkt. Mkilia alisema hayo leo, Machi 1, 2025 mjini Morogoro wakati akifungua warsha na Jukwaa la Wahariri (TEF) yenye lengo la kuwajengea wahariri hao uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda taarifa binafsi za watu.

Dkt. Mkilia alisema, hakuna anayependa taarifa zake binafsi ziwekwe hadharani, hivyo ni jukumu la Tume hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo waandishi wa habari kuhakikisha faragha za Watanzania zinalindwa.
Alisema, kukua kwa teknolojia licha ya kurahisisha mambo mengi, lakini imefanya taarifa binafsi za watu kusambaa kwa kasi hususani kwenye mitandao ya kijamii.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunazingatia ulinzi wa taarifa zetu ili kulinda faragha za watu. Hakuna anayependa ujue anayofanya nyuma ya pazia, hivyo unaweza kuona umuhimu wa jambo hili tunalozungumzia.”
“Tuhakikishe jamii inaelewa umuhimu wa kulinda faragha za watu kwani tupo katika dunia ya Kidigitali,” alisema Dkt. Mkilia.

Awali, akielezea majukumu ya PDPC ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Namba 11 ya mwaka 2022, Dkt. Mkilia alisema ni chombo huru kinachodhibiti na kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi nchini.
Dkt. Mkilia alisema, sheria hii imeanzishwa ili kulinda taarifa binafsi na kujali faragha za watu na inalenga kuweka kiwango cha chini cha matakwa ya ukusanyaji, uchakataji na kuimarisha ulinzi wa taarifa binafsi zinapochakatwa na vyombo vya Serikali na binafsi.
Akielezea zaidi kuhusu taarifa binafsi, Mkurugenzi huyo wa PDPC alisema, ni taarifa yoyote ambayo inaweza kutumika kumtambua mtu au kumtambulisha mtu.

Miongoni mwa taarifa hizo ni jina kamili, kabila, jinsia, elimu, anuani, namba ya simu, barua pepe na namba ya hati ya kusafiria “kwa ufupi hizi ni zile taarifa ambazo ukiziona au ukizisikia basi moja kwa moja zinakupa nafasi ya kumjua, kumtambua mtu.”