Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetoa msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwa wahanga wa athari za mvua katika vijiji vitatu katika wilaya ya Micheweni, Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari 27 Mei, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis alisema, vyakula hivyo ambavyo ni mchele, unga wa ngano, sukari na mafuta ya kula vimetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na wadau wengine.
Mbeto alisema, msaada huo ni sehemu ya utamaduni wa CCM kusaidia jamii pale inapopatwa na changamoto tofauti kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema, wananchi walionufaika na msaada huo ni wa vijiji vya Namapofu, Chunguni na Shumba Mjini, ambao wamekumbwa na kadhia hiyo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha hivikaribuni na maji kujaa majumbani mwao, kutokana na barabara ya lami iliyojengwa kutoka mzunguko wa Micheweni kwenda bandarini.
“Maendeleo huja na changamoto zake kwani barabara ya lami iliyojengwa imekuwa kwa juu kidogo kuliko nyumba za makazi, ndio maana hata mvua ziliponyesha maji yakakosa mwelekeo na kwenda kwenye makazi,” alisema Mbeto.
Mwenezi huyo alisema, wakandarasi wa mifereji walikuwa wanasubiri lami ikamilike na wakati wowote wataanza ujenzi wa mifereji.
“Mkuu wa mkoa kaniambia wakandarasi wakati wowote wataanza ujenzi huo,” alisema mwenezi huyo.
Alisema, Mkuu wa Mkoa na Wilaya wamefanya kazi kubwa hadi sasa na wadau zaidi wanakaribishwa kusaidia wananchi hao, kwa kuwa bado wanahitaji msaada zaidi kwani wamepoteza hadi nguo zao.
Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi ameagiza kitengo cha maafa kufanya tathmini ya kina ya nyumba zilizoathiriwa na kadhia hiyo ili kujua jinsi ya kuwasaidia zaidi.
Mbeto alisema, Rais Dkt. Mwinyi ameguswa na adha hiyo na kwa kushirikiana na baadhi ya wafanyabiashara ndio wamefanikiwa kupata hivyo vyakula na amewapa pole na amewataka wadau wengine kujitokeza kuwasaidia wananchi hao.