SMZ yadhamiria kuleta Mapinduzi makubwa Sekta ya Elimu

0

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Awamu ya Nane imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Elimu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika mkutano na walimu wakuu wa skuli za sekondari, Msingi, maandalizi na wenyeviti wa kamati za skuli kwa Mkoa wa Kusini Unguja uliofanyika katika ukumbi Mkutano wa Dkt. Ali Muhammed Shein Tunguu.

Ameeleza kuwa, Serikali imeamua kuipa kipaumbele sekta ya elimu kulingana na mahitaji ili kuzalisha wataalamu walio bora.

Hemed amewataka walimu wakuu kuwajibika, kufuatilia na kusimamia vyema walimu walio chini yao pamoja na wanafunzi ili kujenga nidhamu na mustakabali mwema.

Alisema, kila mwalimu mkuu lazima asimamie kwa kufuata misingi ya sheria, haki na wajibu ili kufanikisha azma ya serikali ya kutatua changamoto ya elimu kwa mikoa yote ukiwemo mkoa wa Kusini Unguja.

Aidha, Makamu wa Pili wa Rais ameutaka uongozi wa Wizara Elimu kuangalia upya vigezo vya upatikanaji wa walimu wakuu kulingana na sifa, zilizowekwa kisheria ili kuirejeshea heshima sekta ya elimu Zanzibar.

“Kuna walimu wakuu hawana sifa ya kuwa mwalimu mkuu, hana ufuatiliaji hana usimamizi nzuri wala ushirikiano na wenziwe mwalimu kama huyu hafai lazima awajibishwe,” alisema.

Hemed alisema, Wizara ni lazima kuhakikisha wanawasimamia ipasavyo walimu wakuu wote kwa lengo la kuboresha elimu na kuongeza ufaulu ili kupata viongozi bora na wataalamu wa baadae.

Aidha, Makamu wa Pili ameutaka uongozi wa mkoa kushirikiana na kamati za skuli za mkoa kuhakikisha wanaimarisha nidhamu kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa mkoa huu.

“Ni lazima kuhakikisha tunasonga mbele kwenye upasishaji wa wanafunzi kwani serikali imedhamiria kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekata ya Elimu kwa mikoa yote ikiwemo Mkoa wa Kusini Unguja,” alisema.

Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Hussen Ali Mwinyi itahakikisha inatatua changamoto zote za walimu ikiwemo vifaa vya kusomeshea ili kurahisisha ufanyikaji wa kazi kwa maslahi ya Taifa.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha katika ajira mpya za walimu ni vyema kuwapa kipaombele walimu wanaokaa maeneo husika ili kuondosha changamoto za ufanyaji wa kazi.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Muhammed Musa amesema wizara imejipanga kufungua kitado cha tano na cha sita katika skuli ya Hasnuu Makame ili kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wanaofaulu kufata elimu hiyo maeneo ya mbali.

Lela alisema, Wizara hiyo itahakikisha inazitatua changamoto zote zinazowakabili walimu ili yale malengo ya Serikali ya kutoa elimu bora wananchi na kupata wataalamu bora liweze kufikiwa.

Kwa upande wao walimu wakuu na wenyeviti wa skuli za Mkoa wa kusini Unguja wameiomba Serikali kuondosha changamoto zote zinazowakabili walimu wa mkoa huo ikiwemo uhaba wa walimu, uhaba wa vitendea kazi, pamoja na kupatiwa stahiki zao ili kuleta ufanisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here