SMZ yaahidi kuendelea kuwatunza na kuwalinda wazee

0

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza kuwa itaendelea kuwatunza, kuwalinda na kuwapa heshima wazee wa nchi hii, kwa kutambua kuwa wao ni hazina kubwa ya Taifa na wamekuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hassan Ibrahim, katika kongamano la kuadhimisha Siku ya Kupinga Udhalilishaji kwa Wazee Duniani lililofanyika katika eneo la Sebleni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Hassan alisema, Zanzibar ni miongoni mwa maeneo machache duniani yanayotoa kipaumbele kwa ustawi wa wazee kwa kuwapatia huduma, stahiki na heshima wanazostahiki.

“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitarudi nyuma katika kuwatendea haki wazee. Tutaendelea kuwapenda, kuwatunza, na kuwalinda dhidi ya vitendo vyote vya udhalilishaji. Hii ni dhamira ya kweli ya Serikali.”

Amebainisha kuwa zaidi ya Shilingi Milioni 300 zimetengwa kuimarisha mabaraza ya wazee kwa lengo la kuwapa fursa ya kupaza sauti na kusimamia haki zao katika jamii.

Mkurugenzi huyo pia aliwaasa vijana kuwatunza na kuwaheshimu wazee, akiwataka kuepuka vitendo vya kuwadhalilisha ikiwemo kuwatolea lugha chafu, kuwafukuza majumbani, na kuwaita wachawi—vitendo ambavyo vinadhalilisha utu wa wazee.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazee Wastaafu (JUWAZA), Salama Kombo Ahmed, amesema kuwa bado kuna changamoto za udhalilishaji kwa wazee, hasa kwenye maeneo ya huduma kama vile magari ya abiria, hospitali na benki, ambako hukumbwa na usumbufu na ucheleweshwaji wa huduma.

“Wazee wengi wanakaa kwa muda mrefu kusubiri huduma bila kipaumbele, jambo ambalo ni changamoto kubwa kiafya na kiakili,” alisisitiza.

Aidha, aliwahimiza wazee wanaokumbwa na udhalilishaji wasikae kimya bali watoe taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Nao Mzee Issa Kidali Khamis na Fatma Hamza, wajumbe wa Baraza la Wazee la Mkoa wa Mjini, walipongeza juhudi za Serikali na kuomba kuwepo kwa mwakilishi maalum wa wazee katika Baraza la Wawakilishi ili kusimamia haki zao katika ngazi za juu za maamuzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here