MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi mbali mbali katika kuimarisha huduma za lishe na afya bora kwa wananchi.
Ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kisekta wa Lishe Zanzibar 2025-2029 uliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.
Alisema, Serikali inatambua kuwa lishe bora ndio msingi imara wa maisha ya mwanaadamu na ndio tegemeo lenye kuto vijana wenye weledi na nguvu kazi ya kujenga Taifa lenye maendeleo endelevu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema lengo la mpango mkakati huo ni kuimarisha Afya za wananchi na kuondoa changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa lishe bora ikiwemo udumavu wa watoto, uzito pungufu na utapiamlo hususan kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ( 5 ) na wanawake wenye umri wa kuzaa ambao ndio walengwa wakubwa wa mpango huo.
Aidha, Hemed alisema Mpango Mkakati wa Lishe utakuwa ni chachu ya utekelezaji wa mipango mingine kisekta na mikakati mbali mbali ya Serikali inayolenga kuboresha lishe na kuimarisha afya ya jamii, kupunguza maradhi pamoja na kuipunguzia Serikali mzigo mkubwa wa kugharamia matibabu kwa wagonjwa wa ndani na wale wanaosafirishwa nje ya nchi.
Sambamba na hayo Hemed ametoa wito kwa viongozi wa sekata zote husika ambazo zimetajwa katika mkakati huo kufanya wajibu wao ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane (8) katika kuimarisha Afya za wananchi pamoja na kuitaka jamii kufuata utaratibu mzuri wa lishe bora ili kuondokana na chamgamoto mbali mbali za kiafya zinazoweza kuepukika.
Nae Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazurui alisema, ili kuimarisha afya ya mama na mtoto Wizara ya Afya imejipanga kuboresha viashiria vya lishe kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano ( 5 ) mama wajawazito na wananfunzi kwa lengo la kutengeneza jamii yenye Afya na lishe bora kwa maendeleo ya Taifa.
Mazurui alisema, Wizara ya Afya imeanzisha program za lishe katika ngazi ya Mkoa na maskulini ili kutanua zaidi uwelewa kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na lishe bora ili kujenga jamii Imara na yenye lishe endelevu
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkaazi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) Tanzania ELKE WISCH alisema, Ukuwaji mzuri wa mtoto unategemea upatikanaji wa lishe bora ambapo tafiti mbali mbali zinaosnesha kuwa asilimia 70% ya watoto nchini hawakuwi vizuri kutokana na kutopatikana kwa lishe bora kwa mama na mtoto.
Alisema, Mpango mkakati wa Kisekta wa lishe Zanzibar una lengo la kuhakikisha watoto na wajawazito wanafikiwa na huduma za Afya ikiwemo lishe bora ili kuandaa kizazi bora kisicho na changamoto ya udumavu, utapia mlo ma maradhi nyemelezi kwa maslahi mapana ya Zanzibar.
Alisema, uwelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kuwa na lishe bora bado ni mdogo sana hivyo mpango mkakati huo utajikita katika kutoa elimu ya lishe kwa rika zote hasa kwa wanafunzi wa skuli ambao ndio wahanga wakubwa kutokana na ulaji usiofaa.