Sisi ni wamoja, tusiruhusu maneno ya kibaguzi – Dkt. Mwinyi

0

MGOMBEA Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, amewataka Wazanzibar kutoruhusu maneno yatakayosababisha wakabaguana na hatimaye kuvuruga amani.

Dkt. Mwinyi alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 4, 2025 Uvivini, Tumbatu, Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo alisisitiza, bila amani, hakuna maendeleo na hiyo imekuwa ajenda ya kudumu ya chama cha Mapinduzi.

Alisema, kwasasa Wazanzibar ni wamoja, na nchi ina amani na hakuna ubaguzi, hivyo wasikubali ajitokeze mtu yeyote akawatia maneno wakaanza kubaguana kwa rangi, kabila na hata sehemu wanazotoka iwe Kisiwa cha Pemba, Unguja, Kaskazini au Kusini.

“Sisi ni wamoja, tunapaswa kuendelea namna hii ili tuweze kupata amani katika nchi yetu, ili tuweze kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo kuliko ambazo tumezipata,” alisema Dkt. Mwinyi.

Alisema, ukiwasikiliza wapinzani, hawatamki neno amani na mara zote wanazungumza maneno mengi ya kibaguzi, “utawasikia huyo sio Mzanzibari halisi, watasema huyu hakuzaliwa hapa, watasema hiki na kile, sisi tunasema, kila Mzanzibari anaweza akawa na nasaba nje ya Zanzibari na bado ni Mzanzibari.”

Dkt. Mwinyi akifafanua zaidi alisema, wapo Wazanzibari wenye asili ya Ngazija, wengine India na wapo wenye asilia ya Oman, lakini wote ni Wazanzibar na kusisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kuishi bila kubaguana na ndipo wanaweza kudumisha amani katika nchi.

“Kama mnataka kudumisha amani, chagueni chama cha Mapinduzi,” alisisitiza Dkt. Hussein Mwinyi na kuongeza kuwa, chama hicho pekee ndio kinachoweza kusimamia amani nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here