Na Iddy Mkwama
MKURUGENZI wa Shirika na Nyumba la Taifa (NHC) Hamad Abdallah Hamad amesema idadi kubwa ya wanaodaiwa kodi na Shirika hilo ni wale ambao walikuwa wapangaji wao, lakini wamehama kwenye majengo yao.
Alisema, kwasasa wameweka mikakati mbalimbali ya kuwapata wanaokimbia na madeni wakiwemo wenye makampuni ambapo alisisitiza; “sio salama sana kwa kampuni kukimbia deni la NHC, tutawapata.”
Mkurugenzi huyo alisema hayo Juni 16, 2025 jijini Dar es Salaam kwenye Mkutano na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, ambapo alibainisha kwamba, alipoingia kwenye Shirika hilo, alikuta linadai Shilingi Bilioni 27, lakini hivi sasa baada ya kukusanya Shilingi Bilioni 5, deni limebaki Shilingi Bilioni 22.
Alisema, katika kukabiliana na changamoto hiyo ya kukusanya malimbikizo ya madeni sugu, hususani kwa wateja waliohama kwenye majengo ya NHC, wameanza kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Credit Information Reference Bureau na BRELA.
“Tunashirikiana nao ili kuwapata wadaiwa wengine binafsi na kampuni zilizohama kwenye nyumba za Shirika,” alisema na kuongeza kuwa, tangu walipoanza ushirikiano na wadau hao, wamepata mafanikio ambapo wadaiwa wanakwenda wenyewe kulipa.
Alisema, wanapogundua mteja wao amehama bila kulipa kodi, wanapeleka taarifa zake Credit Information Reference Bureau kisha wanampa notisi ya mwezi mmoja, anaposhindwa kulipa anazuiwa kukopa kwenye mabenki.
“Hii imeanza kuzaa matunda, watu wanakuja wenyewe, wanakuja kulipa. Jitihada hizi zimewezekana kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, Msajili wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kukusanya madeni ya Serikali,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi huyo wa NHC alisema, ili kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya wapangaji kukimbia na madeni ya malimbikizo ya kodi, hivi sasa wateja wao wapya wanalazimika kulipa Amana ya Pango (Security deposit) na hadi sasa kwenye akaunti yao wana Shilingi Bilioni 27, ambazo ni za wapangaji ambao wamelipa amana.
“Ni pesa ya tahadhari na kama mtu atataka kuondoka kwenye jengo la Shirika, ni pesa ambazo tunamrejeshea baada ya kuhakikisha hadaiwi na shirika,” alifafanua Mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa, mbali na mikakati hiyo wanaendelea kuchukua hatua kwa wadaiwa wasiozingatia masharti ya mikataba, ambapo wapangaji 150 wamevunjiwa mikataba yao.
Mbali na waliovunjiwa mikataba, Shirika hilo limewapa notisi wadaiwa 100 ya kuhakikisha wanalipa madeni yao kabla ya kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.