‘Sheria ya Huduma ya Habari itafanyiwa marekebisho’

0

Na Mwandishi Wetu

MSEMAJI wa Serikali, Gerson Msigwa, amewahakikishia wadau wa habari nchini kwamba, Sheria ya Huduma ya Habari itafanyiwa marekebisho.

Alitoa kauli hiyo Oktoba 28, 2022 wakati akizungumza na Kituo cha Televisheni cha ITV kuhusu mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Habari ulipofika.

Akizungumza na mtangazaji wa kituo hicho, Godfrey Monyo, Msigwa alisema ‘‘sheria hii (Sheria ya Huduma ya Habari) itafanyiwa marekebisho kama wadau walivyotoa maoni na tutakuja kuwa na sheria nzuri,’’ alisema.

Akisisitiza kauli yake, alisema Serikali haitaki kuacha mdau yeyote nyuma kwa kuwa, lengo lake ni kuunda sheria inayokubalika kwa wote.

Alisema, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari amepanga kukutana na wadau katika hatua ya pili ya mchakato huo.

Msigwa alisema, nia na madhumuni ya kikao hicho ni kupata msimamo wa pamoja kati ya Serikali na wadau wa habari kabla muswada huo haujapelekwa bungeni na Waziri kwa ajili ya kujadiliwa na wabunge na kupitishwa.

Aidha, Msigwa alisema kwamba Serikali ina dhamira ya dhati kuibadilisha sheria hiyo ili iweze kuwa bora zaidi ndiyo maana wameamua kushirikisha wadau wote ili waweze kutoa mapendekezo yao na kujadili vifungu ambavyo wanaona vina shida.

Aliongeza kuwa, baada ya kikao hicho wadau hawatalalamika tena, kwani watakuwa wameshirikishwa kikamilifu katika mabadiliko ya sheria hizo.

‘‘Moja kati ya maeneo Serikali ya Awamu ya Sita imeamua kuyafanyia kazi, ni kuimarisha ama kukuza zaidi uhuru wa vyombo vya habari na kutengeneza mazingira bora ya sekta ya habari ili vyombo vya habari viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi.

“Nafurahi kwamba, mchakato unakwenda vizuri, tumeshakutana na wadau na tumeishapokea maoni yao pia maoni ya Serikali yamekusanywa na sasa kinachoandaliwa ni mkutano ambao utamkutanisha waziri na wadau,’’ alisema Msigwa.

Kwa upande wake wa Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile alisema, ataendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya sheria za habari kwa kushirikisha wadau Wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here