SERIS Foundation watoa msaada wa vifaa kwa watoto wachanga

0

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya SERIS (Seris Foundation) yenye Makao Makuu yake Ilala, Jijini Dar es Salaam, imetembelea na kutoa msaada wa vifaa kwa Watoto Wachanga waliozaliwa usiku wa kuamkia Juni 16 katika Hospitali ya Rufaa ya Amana, ambapo Tanzania na Afrika kwa ujumla inaadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika.

Awali, akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Uongozi wa Hospitali hiyo, Ofisa Muuguzi kiongozi wa Hospitali ya Amana, Vicent Sinkamba ameishukuru taasisi ya SERIS kwa vifaa hivyo, huku akiendelea kuomba wadau kuendelea kujitokeza kusaidia mahitaji muhimu.

“Kwa msaada huu tunashukuru SERIS Foundation utaenda kusaidia watoto wetu wadogo hapa Amana kwani wapo wazazi wanaokuja na mahitaji yao ni madogo, hivyo vinaenda kuwagusa. Pia,vifaa tiba hivi vinaenda kuwa msaada kwa wazazi wengine watakaokuwa wanaendelea kufika hapa kitibiwa.’’ alisema Sinkamba.

Aidha, Sinkamba alisema, usiku wa kuamkia Juni 16, jumla ya Watoto 22 wamezaliwa, ambapo kati ya hao watoto 11 wamezaliwa kawaida na watoto 11 wamezaliwa kwa upasuaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SERIS Foundation, CPA. Deborah Wami amewashukuru uongozi wa Amana kwa kuwapokea na kuahidi kuendeleza mashirikiano katika kuhakikisha wanawafikia watoto Wachanga, katika kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

“Leo siku ya Mtoto wa Afrika wana SERIS Foundation tumetembelea watoto wachanga katika hospitali ya Amana ambapo ni mojawapo ya malengo yetu katika kufikia watoto wachanga wenye umri wa sifuri hadi miezi mitatu.”

Kwa mujibu wa UNICEF, inayoonesha kuwa kwa wastani watoto milioni 2.1 huzaliwa kila mwaka hapa nchini, kati ya watoto hao wanaozaliwa wakiwa wazima wapo na wengine huzaliwa wakiwa na shida mbalimbali ikiwemo upumuaji na shida zingine ambazo zinawasumbua sana watoto wachanga, hivyo SERIS tumejikita katika upande huu.’’ alisema CPA. Deborah Wami.

Aliongeza kuwa, wameona vyema kutupia jicho watoto hao ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali huku gharama zao za matibabu kuwa kubwa kulingana na ukubwa wa tatizo, lakini pia watoto hawa kutokana na mfumo wa bima nchini, baadhi ya watoto hawa hupata bima kwa kuchelewa kidogo na wengine kutopata kabisa.

“SERIS Foundation inatoa wito kwa jamii na Taasisi zingine nchini kuangalia watoto wachanga na matatizo ya kiafya wanayokutana nayo ili kuweza kuokoa maisha ya watoto hawa.”

“Vifo vya watoto wachanga hutokea ndani ya wiki nne baada ya kuzaliwa na Vifo vingi hutokea ndani ya wiki ya kwanza baada ya mtoto kuzaliwa, hivyo SERIS Foundation imejikita kwa watoto hawa kuangalia namna ya kuwawezesha kuokoa maisha yao.’’ alisema CPA. Deborah Wami.

Katika tukio hilo, wamechangia ‘Baby diapers for new babies’ na Fetoscope daipa za watoto pamoja na vifaa tiba vya kumpima mama mapigo ya moyo ya mtoto kabla ya kujifungua.

Aidha, alisema SERIS Foundation wamejikita katika mambo mbalimbali ya kijamii na maendeleo kwa ujumla ikiwemo masuala maji, afya, elimu na mengine.

‘’SERIS pia tunafanya kazi na Wahandisi na Wakandarasi Vijana ambao wamemaliza katika vyuo mbalimbali na hawajui wafanye nini, sisi tunawaunganisha na kuona namna ya kuwaonesha fursa na kupata kuona wenzao nini wanafanya ili kuwasogezea soko la ajira.’’ alisema.

Aliendelea kusema:”SERIS Foundation Inafanya haya katika kuchangia kufikia Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 sambamba na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Hii ni katika maendeleo endelevu ya nchi ikiwa katika kupunguza vifo vya watoto wachanga.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here