Serikali yawekeza kuwainua vijana kuboresha taaluma zao

0

KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdalla Said, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewekeza fedha nyingi katika kujenga vituo mbalimbali vya ubunifu kwa lengo la kuwawezesha vijana kuboresha taaluma na ujuzi wao.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Ubunifu Zanzibar (Zanzibar Innovation Day) yaliyofanyika katika Chuo cha Ubunifu cha IITM Madras, kilichopo Bweleo, Wilaya ya Magharibi ‘B’, Katibu Mkuu amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuifungua Zanzibar kitaaluma na kiuchumi.

“Serikali imewekeza katika miradi ya ubunifu ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kisasa utakaowaandaa kwa ushindani wa kimataifa. Ni muhimu vijana kuchangamkia fursa hizi na kusoma kwa bidii,” amesema Khamis Abdalla Said.

Aidha, amewataka vijana kutumia fursa zinazojitokeza Zanzibar kwa kuongeza ujuzi na ubunifu, akisisitiza kuwa sekta ya teknolojia ina nafasi kubwa katika kuinua uchumi wa vijana.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya India (IITM Zanzibar), Prof. Preeti Aghalayam, amesema chuo hicho kimejipanga kuendeleza vipaji vya wanafunzi wenye uwezo mkubwa katika masomo ya sayansi, teknolojia na hisabati (STEM), ili kuandaa kizazi cha viongozi wa teknolojia barani Afrika.

“Lengo letu ni kuwapa vijana maarifa ya kisasa na kuwajengea uwezo wa kubuni suluhisho bunifu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi,” amesema Prof. Aghalayam.

Wanafunzi wa chuo hicho pia wameeleza kuwa elimu ya ubunifu wanayoipata kupitia IITM Zanzibar itawawezesha kubuni miradi mbalimbali ya kiteknolojia itakayowasaidia kujiendeleza kiuchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here