Na Shaban Juma, WAF-Kilimanjaro
HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC imekuwa mshirika muhimu katika utekelezaji wa sera na mipango ya sekta ya afya kwa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, mafunzo kwa wataalamu wa afya pamoja na kufanya tafiti zinazochangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alipomwakilisha Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa katika maadhimisho ya miaka 55 ya hospitali hiyo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kitengo cha Tiba ya Magonjwa ya Moyo (Cardiac Centre) yaliyofanyika leo Machi 9, 2026 mkoani Kilimanjaro.
“Tunaipongeza hospitali hii ya KCMC kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini tangu kuanzishwa kwake rasmi tarehe 6 Machi 1971 na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” amesema Dkt. Samizi.
Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha ushirikiano na hospitali hiyo kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (Public Private Partnership – PPP) kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Aidha, Dkt. Samizi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kikubwa katika kuimarisha sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zenye ubora unaokubalika.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa Kitengo cha Tiba ya Magonjwa ya Moyo, Dkt. Samizi ameipongeza KCMC kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kufanikisha kuanza kwa mradi huo ambao utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi pamoja na kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Pia, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za kifedha pamoja na Watanzania waliopo ndani na nje ya nchi kuunga mkono juhudi za uchangishaji rasilimali kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa vitakavyotumika katika kitengo hicho.
Mwisho, amesema Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala la muundo wa utumishi (Scheme of Service) unaoendana na hadhi ya hospitali hiyo ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya.