Serikali yasisitiza uzingatiaji wa sheria na ubora katika ujenzi wa shule za Msingi

0

OR- TAMISEMI

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amewataka wakuu wa shule na wenyeviti wa kamati za ujenzi nchini kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni, miongozo na taratibu katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ya msingi.

Akifungua mafunzo ya usimamizi wa ujenzi kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) leo Oktoba 11,2025 mkoani Morogoro kwa niaba ya Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa Elimu ya Awali na Msingi, kutoka Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Abdul Maulid, amesema ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimebainisha mapungufu katika baadhi ya miradi, hivyo viongozi hao wanapaswa kusimamia kikamilifu ili kulinda rasilimali za umma.

Maulid amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mtoto anajifunza katika mazingira salama na yenye miundombinu bora, hivyo utekelezaji wa miradi ya ujenzi lazima ufuate viwango vilivyowekwa.

Alisisitiza kuwa kila hatua ya ujenzi inapaswa kukaguliwa na wataalam wa halmashauri kabla ya kuendelea na kazi ili kuepuka makosa ya kiufundi.

Aidha, amewahimiza kutunza miundombinu inayojengwa na kuendelea kuielimisha jamii kuhusu wajibu wa kuihifadhi na kuweka utaratibu wa ukarabati mdogo kupitia ruzuku za uendeshaji ili kuzuia uchakavu wa mapema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Susan Nussu amesema jumla ya washiriki 3,202 wanahudhuria mafunzo hayo yanayofanyika katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na Mwanza.

Alibainisha kuwa katika miaka ya fedha 2022/23 na 2023/24, Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepeleka Shilingi Bilioni 311.3 kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya elimu, yakiwemo ujenzi wa shule mpya 379 za awali, vyumba 10,462 vya madarasa, matundu 16,180 ya vyoo, majengo 379 ya utawala, mabweni mawili, nyumba 51 za walimu, vichomea taka 379 na ukarabati wa shule 46.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya elimu na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kupitia miundombinu imara na endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here