OR-TAMISEMI, Mwanza
SERIKALI imeahidi kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu ili kuwezesha walimu na wanafunzi kufundisha na kujifunza katika mazingira bora na salama.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 18, 2025 Mkoani Mwanza na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale, wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule za msingi na sekondari yaliyofanyika mkoani humo.
Mtwale amesema ongezeko la idadi ya wanafunzi nchini limesababisha mahitaji makubwa ya miundombinu ya elimu kuanzia ngazi ya awali, msingi hadi sekondari, hivyo Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hizo.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya maboresho ya sera na mitaala ya elimu, ikiwa ni pamoja na kuanza utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne,” amesema Mtwale.
Aidha, alibainisha kuwa kati ya mwaka 2021 na 2025, Serikali imejenga jumla ya shule mpya 2,441, zikiwamo shule za msingi 1,399 na sekondari 1,042 katika maeneo ya vijijini yasiyokuwa na shule au yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi, huku shule kongwe 906 zikikarabatiwa.
Mtwale amewataka wajumbe wa kamati za ujenzi kushirikiana na wenzao kwa kuwapa elimu na ujuzi walioupata ili kuwa na uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Mkwama, amewataka wakuu wa shule kuendeleza mshikamano na kutekeleza kwa ufanisi kazi nzuri zinazofanywa chini ya miradi ya elimu, ikiwemo BOOST, ambayo imeboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Naye Mratibu Msaidizi wa mradi wa BOOST, Reuben Swila, amesema mradi huo umechangia kuongeza kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya masomo.
Aliongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, wanatarajia kujenga darasa maalum kwa ajili ya masomo ya TEHAMA (darasa janja).