Na Clement Robert – WAF, Dar es Salaam
SERIKALI itaendelea kuweka juhudi kubwa zaidi katika kupunguza ajali za barabarani kwa kuelimisha madereva wa pikipiki(bodaboda) na wananchi kwa kampeni yake ya ‘Vaa Helmet Ubongo hauna Spea’ kupitia Wizara ya Afya sehemu ya elimu ya afya kwa umma kama ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na madhara wanayopata Wananchi kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya uendeshaji wa vyombo vya moto
Haya yamesemwa Aprili 12, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt.Grace Magembe baada ya kushiriki matembezi ya mshikamano, yaliyoanzia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu.
Amesema, wagonjwa 7 kati ya 10 wanaopokelewa kwenye taasisi ya mifupa MOI wanakuwa wamepata majeraha kwasababu ya ajali za barabarani, huku asilimia 30 ya ajali hizo zinakuwa zimetokana na pikipiki (Bodaboda)
“Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza ajali za barabarani kwa kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma. Takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya majeruhi wanaopokelewa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) hutokana na ajali za barabarani, ambapo sehemu kubwa inahusishwa na bodaboda, hali inayodhihirisha ukubwa wa tatizo hili na umuhimu wa kuendelea kutoa elimu, kusimamia sheria za usalama barabarani na kubadili mienendo ya watumiaji wa vyombo vya usafiri ili kupunguza madhara yanayoweza kuzuilika,” amesema Dkt. Grace Magembe.
Dkt. Magembe ameongeza kuwa,pamoja kuwa Bodaboda ni miongoni mwa kazi ambazo zimesaidia vijana kujiajiri na kujiongezea kipato, hivyo ameshauri vijana kutumia vyombo hivyo kwa uangalifu kwa kuzingatia Elimu inayotolewa mara kwa mara ili watumie vyombo hivyo kwa usalama wao na wananchi wengine,kwani Usafiri huo unatumika na kuaminika zaidi hasa sehemu ambazo magari na vyombo vingine vya usafiri haviwezi kufika kwa urahisi.
Aidha,Dkt.Magembe amesema kuwa,baada ya matembezi haya ya mshikamano yaliyolenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu afya ya ubongo, mishipa ya fahamu pamoja na mgongo.
Ameongeza kuwa Aprili, 13 mpaka Aprili 15, 2026 kutakuwa na zoezi la kujengeana uwezo kwa wataalam wa afya ndani na nje ya nchi, huku Aprili 16, 2026 kutafanyika ufunguzi rasmi ambapo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi