WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete amesema Serikali itaendelea kuwashirikisha watu wenye ulemavu na kuhakikisha ulinzi wa kundi hilo.
Waziri Kikwete alisema hayo wakati aliposhiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya uelewa kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), zilizofanyika Juni 13, 2025 katika viwanja wa Mwanga Mkoani Kigoma, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Kikwete alisema, maadhimisho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka na yanatumika kukumbushana umuhimu wa kushirikisha wenye ulemavu wa ngozi, Haki zao, umuhimu wa Serikali kuendelea kuangalia maslahi na ulinzi wao.
Katika shughuli ya Mwaka huu, mtandao maalum wa kusajili watu wenye ulemavu unaowezesha usajili kwa njia ya Elektroniki hata kwenye maeneo yaliyo nje ya mtandao ulizinduliwa.

Mfumo huo, unawezesha taarifa za watu wenye ulemavu kuchukuliwa na kuchambuliwa, ambapo zitaiwezesha Serikali kupata taarifa za kina zitakazowezesha kupanga mipango ya maendeleo ikiwemo kuwashirikisha wenye ulemavu.
Waziri Mkuu Majaliwa, akihutubia kwenye hafla hiyo, alitoa maagizo mahsusi kwa wakuu wa Mikoa na wadau waliokuwepo kuhusu matumizi sahihi ya mtandao huo na kuwashirikisha watu wenye ulemavu kwenye masuala mbalimbali likiwemo suala la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.
Waziri Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha watu wenye Ualbino kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo.
