Na Mwandishi Wetu
NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amewahakikishia wadau wa habari kwamba, Serikali itakamilisha mchakato wa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari.
Kwenye kikao chake na wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), Novemba 21, 2022, jijini Dar es Salaam Nape alisema, Serikali imepokea maoni yao kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.
”Niwahakikishie kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, inayo nia ya dhati katika jambo hili. Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua,” alisema.
Kikao hicho cha pili cha Wadau wa Kupata Habari (CoRI) na Serikali cha kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, kiliongozwa na Nape mwenyewe. “…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,”
Nje ya kikao hicho, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema kuna muelekeo mzuri wa mabadiliko ya sheria ya habari.
‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na Serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.
‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’ alisema Balile.