RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa taasisi za dini zenye shule pamoja wamiliki binafsi kutoa ushirikiano katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho.
Rais Samia ametoa wito huo leo kwenye Baraza la Iddi el- Fitri lililofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).
Aidha, Rais Samia amezitaka taasisi hizo kuhakikisha stadi zinazotolewa zinasadifu malengo ya sera na ya serikali huku zikiendelea kuwalea wanafunzi kwenye mafunzo ya elimu ya dunia na akhera ili kuwafanya wawe wenye maadili na hofu ya Mungu.
Vile vile, Rais Samia alisema lengo la marekebisho ya sera hiyo ni kuhakikisha elimu inatolewa kwa wote na kuwawezesha kutoa mchango kwenye jamii kwa mazingira ya kisasa pindi wanapohitimu.
Kwa upande mwingine, amewataka wananchi kuendelea kulipa kodi ili Serikali ikusanye mapato kwa haki yatakayoiwezesha kutimiza wajibu wake ikiwemo kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kijamii.
Pia, amekemea tabia ya baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa mbinu mbalimbali ikiwemo kutokutoa risiti au kutoa risiti za kiasi pungufu na kwa wanunuzi wa bidhaa kutokudai risiti.
Rais Samia alisema, Serikali inaweza kuimarisha zaidi huduma za jamii ikiwa itafanikiwa kukusanya zaidi na kupunguza ukwepaji wa kodi kwa kuzingatia idadi ya Watanzania na kiwango cha biashara zinazofanyika nchini.