RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inatambua mchango wa Jumuiya za Watanzania wanaoishi nje ya Nchi (Diaspora) kwa kuwekeza nchini Tanzania na kuisemea nchi kwa kuhamasisha utalii kwa wageni.
Rais Dkt. Mwinyi alisema hayo alipozungumza na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uingereza katika ukumbi wa Hoteli ya Copthorne Tara Hotel London Kensington, Jijini London nchini Uingereza Aprili 6, 2025.

Rais Dkt.Mwinyi amewahakikishia kuwa Serikali itakuwa pamoja nao kuzifanyia changamoto zao zinazowakabili kwa maendeleo ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa Diaspora kuendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja katika hati fungani za Zanzibar SUKUK.
Vilevile, Rais Dkt Mwinyi amefahamisha Serikali kuwatumia wataalamu wa fani mbalimbali wanaoishi nje ya Tanzania kuja kufanya kazi nchini.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza suala la kuendeleza utamaduni, mila na desturi kwa vijana wa kitanzania na kutoiga mila za kigeni.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Mwinyi ameizindua tovuti maalum ya Tanzania Link Portal ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, itakayotoa fursa za biashara, uwekezaji, ufadhili wa elimu ya juu na ajira.