Sababu za Bandari ya Dar es Salaam kuwa kivutio kwa wafanyabiashara

0

Na Mwandishi Wetu

BANDARI ya Dar es Salaam ni lango kuu la Kibiashara; inahudumia nchi jirani zisizo na bandari kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Zimbabwe.

Aidha, Bandari ya Dar es Salaam ni kiungo kikuu cha kibiashara si tu kutoka na kwenda nchi za Afrika Mashariki na kati, bali pia nchi za Mashariki ya Kati, Mashariki ya mbali, Ulaya, Australia na Marekani.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho anasema, moja ya mambo ambayo yanaifanya bandari hiyo kuwa kivutio na kutumiwa na wafanyabiashara wengi, ni kutokana na uwezo wake wa kuingiza shehena na kutoa kwenda sehemu mbalimbali.

Kwa maana kwamba, meli zinazoingia nchini kuleta shehena, zinapotaka kuondoka zinapata shehena ya kusafirisha, jambo ambalo halipatikani kwenye bandari nyingine zilizopo nchi za jirani.

“Bandari yetu ina uwezo wa kuingiza mizigo na kutoa, kila siku asubuhi kuna wastani wa meli 5 hadi 7 zinaingia kule nje, zilikuwa na uwezo wa kwenda kwenye bandari nyingine, lakini zinakuja huku, wanaaangalia wepesi wa ufanyaji wa biashara,” anasema Mrisho.

Anasema, meli ikisubiri nje ina uhakika wa kupata shehena ya kuondoka nayo na kikubwa ni uwezo wa kuzifikia kwa urahisi nchi ambazo zinapakana na Tanzania “kuna Copper kutoka Kongo na Zambia inakuja Dar na ina uhakika wa kuondoka, hiyo ndio biashara na huo ndio uchumi.”

Mrisho anasema, kwa sasa wanaendelea na mipango ya uwekezaji na wana uhakika Bandari ya Dar es Salaam itafanya vizuri zaidi ya nyingine zilizopo nchi za jirani “Dar Port inafanya vizuri zaidi kuliko zilizopo nchi za jirani.”

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali ikiwemo Tovuti ya bandari ya Dar es Salaam, bandari hiyo ina magati ya shehena mchanganyiko (0-5) kwa ajili ya shehena kavu na magari. Magati ya makasha (5-11), vihenge vya kuhifadhia nafaka (silos) vyenye uwezo wa tani 30,000, vituo vya makasha vya nchi kavu (ICD) vyenye uwezo wa kuhifadhi 24,300 TEUs na CFs yenye uwezo wa kutunza magari 6,000 kwa wakati.

Bandari ya Dar es Salaam ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya tani Milioni 18 za shehena kama ifuatavyo:- Shehena za kawaida tani Milioni 5.2, Makasha tani Milioni 6.8 na Vimiminika tani Milioni 6.0

Kwa upande mwingine, kuna eneo la gati lenye urefu wa Mita 2,600 ambalo limegawanywa kama ifuatavyo:- Kitengo cha Shehena Mchanganyiko. Sehemu hii ya bandari ina gati la urefu wa mita 797 lenye mgawanyiko wa magati makuu manne (4), maghala ya kuhifadhia shehena zinazopitia kwenda nchi nyingine yenye ukubwa wa mita za mraba 64,463.5 na hifadhi ya wazi yenye ukubwa wa meta za mraba 201,613.

Bandari ya Dar es Salaam ina Vituo viwili (2) vya Makasha vinavyoendeshwa na TPA Yaani; Kitengo cha Makasha I (Gati Nambari 5 hadi 7) na Kituo cha Pili cha Makasha (Gati Nambari 8 hadi 11). Terminal II ya Kontena ina urefu wa mita 725 na uwezo na uwezo wa kushughulikia zaidi ya TEU 660,000 kwa mwaka kulingana na, miongoni mwa mengine, aina ya vifaa vilivyotumwa, Mifumo ya TEHAMA.

Mbali na hilo, Bandari ya Dar es Salaam ina miundombinu ya kisasa ya kushughulikia shehena ya nafaka. Mifumo iliyopo pamoja na vihenge inapokea tani 30,000 za nafaka.

Kutokana na mifumo hiyo, nafaka inaweza kupakuliwa na kujazwa kwenye magunia kwenye eneo la gatini kwa wastani wa zaidi ya tani 2,000 kwa saa 24 au kuhamishwa kwa kutumia malori. Vihenge vipo katika hali inayotakiwa kimataifa ya uhifadhi nafaka.

Kuna maeneo mawili yanayotumika kupakua shehena ya mafuta. Kuna Single Point Mooring (SPM) na Kurasini Oil Jetty (KOJ). Katika eneo la SPM meli ya mafuta hushusha karibu na ufukwe. SPM ina uwezo wa kupokea meli za mafuta zenye uzito hadi tani za metriki 150,000 (MT) na kasi ya kupakua ya kiwango cha mita za ujazo 2,500 kwa saa kwa mafuta ghafi.

SPM imeunganishwa na viwanda vya kusafishia mafuta vya Dar es Salaam na Ndola – Zambia, Eneo jingine ni la Kurasini, KOJ ambalo uhudumia shehena za mafuta yaliyosafishwa ina uwezo wa kusukuma tani 750 kwa saa. Linaweza kushughulikia meli za mafuta hadi zenye tani 45,000 (MT).

Jambo jingine, Bandari ya Dar es Salaam inahudumuiwa na boti maalum za kuvutia meli (Tugs), boti za nahodha na boti za ulinzi/doria. Pia, kuna miundombinu ya kuelekezea meli bandarini (Navigation Aids). Miundombinu hiyo ni pamoja na maboya, milingoti ya kuongozea meli, alama za ishara na minara ya taa.

Vyombo vikuu vya kuhudumia shehena za kawaida ni winchi kubwa, foko, trekta, matela, grabs, hoppers, Bagging units, malori, mizani, na mikanda ya kuhamishia mizigo. Bandari ina vifaa vya kuhudumia makasha kama vile winchi kubwa (Ship to shore gantry cranes – SSGs).

Vingine ni winchi kubwa za matairi (Rubber tyred gantry cranes RTGs) na winchi kubwa inayotembea katika reli (Rail Mounted Gantry Crane RMG), Gottwalds, malori ya usafirishaji malori yenye foko, matela yanayotumika barabara kuu, matrekta na matela.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here