Rekodi ya Utalii yavunjwa Kilwa

0

Na Beatus Maganja

REKODI ya idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia na Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Machi 4, 2024 imevunjwa baada ya kupokea meli ya nane kutia nanga Hifadhini humo ikiwa na watalii 125 kutoka Mataifa mbalimbali na hivyo kufikisha jumla ya watalii 925 waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Februari 3, 2024.

Kwa mujibu wa takwimu za idadi ya watalii wa kigeni waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha hivi karibuni mwaka 2024 umetajwa kuwa ni mwaka wenye mafanikio makubwa kwa TAWA kupata safari nyingi za meli za watalii kupitia Hifadhi hiyo yenye urithi wa kihistoria na kiutamaduni, ukongwe wa magofu ya kale yaliyojengwa kwa ustadi mkubwa kiasi cha kustaajabisha na kuvutia watalii mbalimbali wanaotembelea hifadhi hiyo

Imeelezwa kuwa takwimu za miaka mitatu kuanzia mwaka 2022, idadi ya meli zilizotia nanga hifadhini humo zilikuwa mbili (2) zikiwa na zaidi ya watalii 200, ambapo mwaka 2023 meli 3 ziliwasili katika hifadhi husika zikiwa na zaidi ya watalii 300 na mwaka huu wa 2024 meli zipatazo nane zikiwa na zaidi ya watalii 900 zimetia nanga hifadhini humo.

Ongezeko hilo la watalii katika Hifadhi hiyo ni ishara kuwa utalii wa malikale unazidi kuchechemka nchini ukichagizwa na jitihada za dhati zilizofanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuitangaza Nchi yetu na vivutio vyake kupitia filamu maarufu ya Tanzania ‘The Royal Tour’ iliyoleta matokeo makubwa kwa muda mfupi.

Pia, nguvu kubwa ya kuwekeza katika kuboresha miundombinu wezeshi ya utalii iliyofanywa na Serikali kupitia TAWA ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo lakini bila kusahau mchango mkubwa wa Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii wa Nchi yetu.

Hii ni dalili tosha kuwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020 na malengo ya Serikali ya kufikisha idadi ya watalii Milioni 5 na mapato ya takribani Dola Bilioni 6 ifikapo mwaka 2025 yanakwenda kufikiwa kwa kishindo na TAWA ikiwa ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki katika kuchangia kufikia malengo hayo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here