REA yataja vigezo vya kuwapata wakandarasi wa miradi ya kusambaza umeme

0
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Hassan, Saidy.

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA); Mhandisi, Hassan, Saidy amesema kuanza sasa kigezo kimojawapo kitakachotumika kuwapata Wakandarasi wanaotekeleza Miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini ni taratibu zote za Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na utendaji madhubuti (Performance) na si vinginevyo.

Mhandisi, Hassan Saidy ameyasema hayo wakati wa mkutano maalum kati ya REA na Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Jijini, Dar es Salaam.

Mhandisi Saidy alisema, mkutano huo maalum ulilenga mambo mbalimbali, moja ni kuwakumbusha Wakandarasi hao kuhusu wajibu wao wakati wa utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini pamoja kujipanga kwa ajili ya kukamilisha Mradi mkubwa wa REA III (Mzunguko wa Pili) ambao unatarajia kukamilika Mwezi Juni, 2024 ambapo imeelezwa kuwa vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme.

Aliongeza kuwa, mkutano huo pia ulikuwa na lengo la kuwakumbusha kuhusu wajibu wao na nafasi zao kwenye Miradi ya usambazaji wa umeme vijijini na kuongeza kuwa pamoja na vigezo vya manunuzi ya zabuni kuwa vitazingatiwa ili kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza Miradi hiyo, suala ya utendaji kazi bora, utakuwa kigezo muhimu kuanzia sasa.

“Tumewaambia kwamba ili Mkandarasi aweze kupata Mradi wa REA, pamoja na vigezo vyote vya Sheria ya Manunuzi ya Umma kuvifikia, lakini tutaangalia “performance” yake kwenye Miradi yetu, sisi wenyewe, kwa hiyo kama Mkandarasi atakuwa anasua sua na kufanya kazi vibaya, hatakuwa na nafasi ya kupata mkataba mwengine.” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu.

Wakati huo huo, Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu walitumia mkutano huo kutoa nishani na vyeti maalum kwa Wakandarasi waliofanya vizuri.

Mhandisi Hassan Saidy alisema, REA iliamua kuwatunuku nishani na vyeti Wakandarasi wanaofanya vizuri kwenye usambazaji wa nishati ya umeme vijijini.

“Tumeona hii ni njia nzuri ya kuwafanya waongeze nguvu, kwenye utekelezaji wa Miradi ya usambazaji wa nishati ya umeme vijijini, tumeona wale wanaofanya vizuri basi tuwatambue, hatuwezi wote tukawa tunawachukulia sawa, Mkandarasi aliyefanya vizuri sana na Mkandarasi anayesuasua hawako sawa, tumfanya hivi ili kuwafanya wahamasike na wafanye kazi vizuri zaidi”. Amesisitiza Mkurugenzi Mkuu, Mhandisi, Hassan Saidy.

Wakandarasi waliofanya vizuri na kutunukiwa nishani ni pamoja na kampuni ya STEG International Services ya kutoka Tunisia, kampuni ya pili ni China Railway Construction Electrification Bureau Group CO, kutoka China, kampuni ya tatu ni Sengerema Engineering Group Ltd ya Tanzania na kampuni ya nne ni Sagemcom Energy and Telecom Tanzania LTD ya kutoka Ufaransa na kampuni ya tano katika kundi la wakandarasi waliofanya vizuri ni CEYLEX Engineering (PVT) Ltd kutoka Sri Lanka.

Wakandarasi waliotunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao na uwajibikaji wao mahili ni pamoja na STEG International Service (Tunisia); China Railway Construction Electrification Bureau Group CO (China); Giza Cable Industries (Misri); Sengerema Engineering Group Ltd (Tanzania) na Sagemcom Energy and Telecom Tanzania LTD (Ufaransa).

Wengine ni OK Electrical & Electronic Services Ltd (Tanzania) na JV White City International Contractors & GuangDong Jianneng Electric Power Engineering Co, Ltd (Tanzania & China); DERM Group (T) Ltd; CEYLEX ENGENEERING (PVT) Ltd; CRJE-CTCE CONSORTIUM (China) na JV SILO Power & GUANGZHOU YIDIAN EQUIPMENT INSTALLATION Ltd (China).

Mhandisi Saidy aliongeza kuwa, REA imeutumia mkutano huo kuwakumbusha Wakandarasi kuhusu viwango vya ubora kwa vifaa (Materials) wanazotumia kwenye ujenzi wa miundombinu ya Miradi ya umeme vijiji, vifaa hivyo ni pamoja na nguzo, nyaya pamoja vifaa vingine “Miradi ya nishati ya umeme vijijini ni Miradi ya Serikali hivyo ni lazima Wakandarasi wafuate vigezo, masharti na maadili.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here