Rais wa Korea Kusini akanusha kuwatukana wabunge wa Marekani

0

SEOUL, Korea Kusini

RAIS Yoon Suk-yeol wa Korea Kusini amesema, ripoti za vyombo vya habari kuhusu matamshi aliyotoa wakati wa safari yake mjini New York, si sahihi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, ilidaiwa Rais wa Korea Kusini alinaswa akiwaita wabunge wa Marekani “wapumbavu” na kusema, wanaweza kumwaibisha rais wa nchi hiyo Joe Biden kwa kutoidhinisha ufadhili wa fedha kwa ajili ya mipango ya afya duniani.

Rais huyo wa Korea Kusini alisema: “Ikiwa wanaharamu hawa katika bunge hawataidhinisha, maskini (Rais wa Marekani Joe) Biden ataonekana mbaya sana.”

Katika mkutano wake wa hivi karibuni na rais wa Korea Kusini, Joe Biden alimuahidi Yoon Suk-yeol kwamba serikali ya Marekani, ikiwa itaidhinishiwa na bunge la nchi hiyo, itachangia Dola Bilioni 6 kwa operesheni za Kimataifa za kupambana na ukimwi, malaria na kifua kikuu.

Shirika la habari la Reuters, likimnukuu Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yol linasema, taarifa za uwongo za vyombo vya habari kuhusu matamshi yake pembeni ya mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa zilipangwa kuharibu uhusiano kati ya Seoul na Washington.

Ofisi ya rais wa Korea Kusini imejaribu kudhibiti suala hilo kwa kusema kwamba, Yoon hakuwa akimaanisha viongozi waliochaguliwa wa Marekani.

Msemaji wa serikali ya Korea Kusini alisema, Yoon Seok-yul hakumtaja Biden kwa jina na kwamba neno alilotumia pengine linafanana kifonetiki na Biden.

Lakini, mkuu wa chama cha upinzani nchini Korea Kusini cha kidemokrasia alisema, hoja zilizotolewa na ofisi ya rais hazina msingi na kwamba, wanachofanya viongozi wa Seoul ni kujaribu kujinasua kwenye kinamasi cha janga la kidiplomasia.

Hayo yamejiri huku ripoti kutoka nchini Korea Kusini zikieleza kwamba umashuhuri wa Yoon Suk-yol umeanza kupungua tangu lilipoibuka sakata hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here