RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Taasisi za umma na sekta binafsi kushirikiana na Wakala ya Taifa ya huduma za ugani (NAESA) ili iweze kufanya kazi na kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Rais Samia ameyasema hayo Agosti 08,2026 wakati akifunga Maonesho ya kitaifa na kimataifa ya NaneNane yaliyofanyika kitaifa Mkoani Dodoma na kwenye kanda nyingine mbalimbali nchini.
“Mtakumbuka pia kwamba nilipotembelea maonesho haya mwaka jana nilisisitiza kuimarishwa kwa huduma za ugani nchini ili ziwafikie wakulima wengi na kwa ufanisi zaidi hivyo nafurahi kwamba sasa tumefikia hatua ya kuanzisha kwa wakala wa huduma za ugani za kilimo kwa ufupi NAESA ulioanza kazi mwezi julai mwaka huu na tayari leo nimezindua na kukabidhi magari 48 kwa awamu ya kwanza yakayaoenda kutumiwa kutekeleza majukumu ya wakala hiyo,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia ameonesha kuvutiwa na kauli mbiu ya maonesho hayo kwa mwaka huu ambapo amebainisha kuwa hatua ya kutambua soko ndo iliongeza uwekezaji wa Serikali kwenye baadhi ya mazao ya sekta za Kilimo na Uvuvi na matokeo yameonekana.
Awali akieleza mafanikio yaliyopatikana kupitia sekta za Mifugo na Uvuvi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa ametaja kukamilika kwa ujenzi wa bandari ya Uvuvi iliyojengwa Kilwa Masoko mkoani Lindi na kugharimu takribani Bilioni 280.58 kama moja ya mafanikio makubwa zaidi huku akisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa ni kitovu cha kukua kwa sekta ya Uvuvi nchini.
“Na hapa nikuombe Mhe. Rais kwa ridhaa yako na kulingana na ratiba yako wakati wowote kuanzia sasa sisi tuko tayari kukupokea Kilwa Masoko uzindue bandari hii ya kisasa” ameongeza Balozi Dkt. Bashiru.
Maonesho ya kitaifa na Kimataifa ya NaneNane kwa mwaka huu yalibebwa na kauli mbiu isemayo “Tambua Soko, Zalisha kwa Tija, Kutekeleza Dira 2050.”