Na Lusajo Mwakabuku – WKS
RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu Prof. Remy Ngoy Lumbu la kuitaka nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 77 utakaojumuisha nchi wanachama wa kamisheni ya Umoja wa Afrika wa Haki za Binadamu na watu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Rais Samia ameridhia ombi hilo lililotolewa na Prof. Lumbu aliyefika Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na Rais na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu masuala ya Haki za Binadamu na Watu huku akiambatana na wadau wa asasi za kiraia za kutetea haki za binadamu za hapa nchini.
Awali, kabla ya kuwasilisha ombi hilo, Prof. Lumbu alianza kwa kupongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza ambapo makundi mbalimbali yameonekana kupewa nafasi ya kujieleza yakiwemo makundi ya wanasiasa, Pia aliongelea suala la uhuru wa vyombo vya Habari ambao unaonekana kuimarika na jitihada mbalimbali zilizofanyika katika kukuza matumizi ya Lugha ya Kiswahili.
Baada ya pongezi hizo Prof. Lumbu aliwasilisha ombi hilo rasmi kwa Rais huku akimuomba pia kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ambapo Mhe. Rais aliahidi kutoa jibu baadae juu ya hilo.
Akiongelea suala la maendeleo ya haki za binadamu, Rais Samia alisema anaamini kuwa matatizo ya ndani yanaweza kumalizwa na sisi wenyewe na sio mtu wa nje na ndio maana alifikia hatua ya kukutana na vyama vya upinzani na kuangalia changamoto ni nini na baada ya majadiliano ikafikia hatua ya maridhiano yaliyopelekea pande zote kuwa kauli moja na hivyo kuondoa migongano.