Rais Samia aifanya Tanzania kuwa kinara wa kuwavutia watalii 2024

0

Na John Mapepele, Dodoma

MAONO makubwa na falsafa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Sekta ya Utalii nchini yameendelea kuleta mafanikio lukuki kwenye anga za Kitaifa na Kimataifa kila uchao huku wakati tunaumaliza mwaka Tanzania ikiendelea kung’ara na kuwa ndiyo nchi inayoongoza kuwavutia watalii Barani Afrika kwa mwaka 2024.

Hii inatokana na Serikali ya Tanzania kupewa tuzo nne na taasisi maarufu duniani kwa utoaji wa tuzo za sekta ya utalii, Taasisi ya Tuzo za Dunia za Utalii Kanda ya Afrika (World Travel Awards Africa – Gala) kwenye usiku wa tuzo uliofanyika kwenye jiji la Mombasa nchini Kenya, Oktoba 18, 2024 ambapo Tuzo ya kwanza ikiwa ni hiyo ya kuwa “nchi inayoongoza kuwavutia watalii Barani Afrika kwa mwaka 2024.”

Tuzo nyingine ilikwenda kwa Bodi ya Utalii ya Tanzania kupewa tuzo ya kuwa “Bodi Bora inayoongoza Barani Afrika kwa mwaka 2024” ambapo Naibu Katibu Mkuu nayeshughulikia eneo la utalii, Nkoba Mabula ndiye aliyeiongoza ujumbe wa Serikali ya Tanzania Mombasa, nchini Kenya kupokea tuzo hizo.

Ni ukweli usiopingika kuwa, dunia imeendelea kushuhudia kwa mara nyingine Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikivunja rekodi na kuandika historia ya kipekee duniani kwa vivutio vyake viwili kushinda tuzo kubwa za utalii barani Afrika tena kwa mara sita kila mmoja mwaka huu 2024!

Zanzibar nayo imetangazwa kuwa eneo maridhawa kwa Matukio na Matamasha (African’s Leading Festivals and Events Desnation 2024), na wadau wengine kama hoteli ya Kifahari ya Thanda iliyojengwa kwenye Kisiwa cha Shungimbili huko Mafia ikiendelea kushinda mara sita katika tuzo ya kundi la hotel ya kifahari iliyopo kwenye Kisiwa Barani Afrika 2024 yaani African’s leading luxury Island 2024.

Tuzo ya tatu na ya nne kwa Serikali zilikwenda kwa Hifadhi za Serengeti na Mlima Kilimanjaro ambapo Mlima Kilimanjaro umeshinda tuzo hii ya kivutio Bora Barani Afrika mara sita kuanzia mwaka 2013, 2015, 2016,2017, 2018 na 2024 wakati Hifadhi ya Serengeti nayo ikishinda mara sita mfululizo kuanzia mwaka 2019. Hivyo Tanzania kuandika historia ya “Sita Kubwa za Sekta ya utalii kwa mwaka 2024”!

Akikabidhi tuzo hizo, Mwanzilishi wa Taasisi ya World Travel Awards Africa- Gala, bwana Graham Cooke alifafanua kuwa taasisi yake imetangaza Hifadhi mbili za Tanzania (Serengeti na Mlima Kilimanjaro) kuwa washindi kwenye kipengele cha Hifadhi na Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2024 ambapo Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kuwa mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora Barani Afrika (Africa’s Leading National Park 2024) wakati Mlima Kilimanjaro ikitangazwa Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika (African Leading Tourism Attraction 2024)

Hifadhi ya Serengeti imezishinda hifadhi nyingine kwa ubora barani Afrika ilizoshindanishwa nazo ambazo ni Maasai Mara ya nchini Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana, Etosha ya Namibia na Kidepo Valley ya nchini Uganda.

Mlima Kilimanjaro umevishinda vivutio vingine vya utalii ambavyo ni Hifadhi ya Ngorongoro, Hartbeespoort aerial Cableway, V&A, Waterfront, Robben Island, Table Mountain zote za Afrika Kusini. Pia Ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, na Pyramid of Giza ya Misri.

Hivi karibuni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana akiwa kwenye maadhimisho ya miaka sitini ya Hifadhi ya Mikumi na Ruaha pia wakati wa kukabidhi kikosi maalum cha wapiganaji wa Jeshi la JWTZ kupandisha Mwenge wa Uhuru na Bendera ya Taifa kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuitangaza Sekta ya Utalii duniani kupitia Filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania.

Ametoa wito kwa watanzania kuunga mkono jitihada za Serikali za kutangaza utalii kwa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kutangaza Tanzania iliyoratibu Filamu ya Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania amefafanua kuwa Wizara itaendelea kusimamia kikamilifu Sera ya Utalii na kutangaza vivutio vya utalii kimkakati duniani ili sekta iweze kuchangia kwenye uchumi wa Tanzania.

Hivi sasa Sekta ya Utalii inachangia takribani asilimia 17 kwenye pato la taifa na takribani asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo kutokana na kuimarika kwa vivutio vya utalii idadi ya watalii kutoka nje imeongezeka kutoka 922,692 mwaka 2021 hadi kufikia watalii 1808,205 mwaka 2023 sawa na ongezeko la takribani asilimia 95.

Kwa upande wa mapato yameongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 1,254.4 kwa mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Kimarekani Milioni 3,373.83 mwaka 2023.

Kwa idadi hii Tanzania imevunja rekodi ya kufikia Idadi ya juu zaidi ya watalii kuwahi kufikiwa lakini pia kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii(UNWTO) kwa ongezeko hilo Tanzania imekuwa nchi ya pili Afrika baada ya Ethiopia na ya 11 duniani miongoni mwa nchi zilizoongeza watalii wengi baada ya Uviko -19 hasa ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2019 kabla ya Uviko -19.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here