Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekabidhiwa Tuzo ya Uongozi wa Kimageuzi Afrika (African Leadership Award 2022), kutoka taasisi ya Afrimma ya Mjini Dallas, Marekani kwa kutambua mchango wake katika sanaa nchini Tanzania.
Tuzo hiyo imepokewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, usiku wa kuamkia leo mjini Dallas, ambapo mwakilishi huyo alisema, Rais Samia katika kipindi kifupi cha uongozi wake, amefanya mageuzi mengi katika sekta ya sanaa ikiwemo kurejesha tuzo za muziki na kuboresha mifumo ya mirabaha ili kuwainua wasanii.
Awali, mamia ya mashabiki waliohudhuria tuzo hizo walimshangilia kwa nguvu Rais Samia alipoonekana katika baadhi ya vipande vya filamu ya ‘Royal Tour’ vilivyokuwa vikioneshwa kabla ya kutolewa tuzo hiyo.
Viongozi wengine wakuu wa Afrika waliowahi kutwaa Tuzo hiyo ni Rais Ian Khama wa Botswana (2015) na Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria (2017).
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa Rais Samia kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake kwenye sekta mbalimbali, ambapo miongoni mwa tuzo alizowahi kukabidiwa tangu alipoingia madarakani; ni tuzo ya Babacar Ndiaye (2022), iliyotolewa Accra, nchini Ghana.
Tuzo hiyo ilitolewa kutokana na mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo hutolewa kwa Mkuu wa nchi iliyofanya vizuri.
Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Rais Samia alisema anajisikia faraja kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kupokea tuzo hiyo, kwani ni heshima kwake na heshima kwa kile anachokifanya katika nchi yake.
Pia, Jumuiya ya Kimataifa ya Watetezi na Amani ilimtangaza kuwa mshindi wa tuzo mbili za Kimataifa ikiwemo ya amani duniani 2022.
Tuzo nyingine aliyotangazwa kuwa mshindi ni tuzo ya Rais wa Dhahabu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, ambapo ni Rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kuipata.
Mbali na tuzo hizo, Rais Samia amepokea tuzo ya heshima ya Pyne Africa Awards 2022 katika hafla iliyofanyika jijini Lagos, Nigeria.
Rais Samia alitunukiwa tuzo hiyo baada ya kuchaguliwa kama Rais bora mwajibikaji katika kuiendeleza sekta ya utalii barani Afrika Tuzo hiyo ilipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana kwa niaba ya Rais.
“Tumeona Rais Samia akipokea tuzo kila mara, zipo nyingi sana nadhani ataweka historia ya aina yake; kuwa Rais mwenye tuzo nyingi barani Afrika kutokana na uongozi wake na jitihada anazozifanya za kuijenga nchi yake,” alisema Aloyce Mlaponi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).