RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar inahitaji fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo Uchumi wa Buluu, sekta ya miundombinu, afya pamoja na fursa za kibiashara kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa za karafuu na mazao ya baharini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mbarouk Nassor Mbarouk, aliyefika Ikulu Zanzibar, Agosti 19, 2025 kumuaga baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa sera ya diplomasia ya uchumi ndiyo iliyopewa kipaumbele hivi sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo ni vema Balozi huyo kuifanyia kazi sera hiyo ili uchumi wa Tanzania hususan Zanzibar uendelee kuimarika.
Naye Balozi Mbarouk amemhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kwamba ataendelea kuimarisha zaidi mahusiano pamoja na kutafuta fursa mbalimbali za ushirikiano.