RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, moja ya alama muhimu za maendeleo ya Taifa lolote ni ubora wa Elimu ya Juu yenye uwezo wa kuzalisha wataalamu wanaoweza kuhimili changamoto za Karne ya 21, hususan katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Disemba 20, 2025 alipohutubia Mahafali ya 21 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), yaliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.
Ameeleza kuwa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, ambacho ni chuo kikuu cha umma, kinaendelea kuwa kitovu na mwanga wa maarifa kwa Taifa, kwa kuwa ni tegemeo la kuzalisha wataalamu, wabunifu, wanasayansi, watafiti, walimu, madaktari na viongozi wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa SUZA imefanya kazi kubwa ya kuongeza idadi ya wanafunzi waliosajiliwa kutoka 2,365 mwaka 2024 hadi kufikia 2,420 mwaka 2025, jambo linaloonesha kukua na kuimarika kwa chuo hicho.
Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amepongeza uongozi wa SUZA pamoja na wahadhiri kwa juhudi zao za kutoa elimu bora na kukifanya chuo hicho kuwa kichocheo cha mabadiliko ya jamii na miongoni mwa vyuo vinavyotambulika katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameleeza kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo ujenzi wa maabara, maktaba, dakhalia na mifumo ya TEHAMA, sambamba na kuimarisha tafiti, ubunifu na uvumbuzi, pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu na watafiti wa ndani na nje ya nchi.
Rais Dkt. Mwinyi, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, ametoa wito kwa SUZA kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii na kuinufaisha Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, pamoja na kuwa tayari kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Serikali.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Shilingi bilioni 33.3 mwaka wa fedha 2024/2025 hadi Shilingi bilioni 37.94 mwaka 2025/2026.
Aidha, idadi ya wanafunzi waliopata mikopo upande wa Zanzibar imeongezeka kutoka wanafunzi 1,093 mwaka 2024/2025 hadi wanafunzi 1,725 mwaka 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 63.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 2,536 wametunukiwa shahada katika ngazi mbalimbali ikiwemo vyeti, stashahada, shahada za uzamili na shahada za uzamivu kwa mwaka wa masomo 2024/2025, ambapo wanawake ni 1,614 na wanaume 922.