RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Waislamu na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuiombea nchi amani na kudumisha mshikamano, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Julai 4, 2025, alipotoa salamu zake kwa waumini wa dini ya Kiislamu mara baada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Sunna Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika hotuba yake Rais Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuwa na dhamira ya kweli ya kudumisha na kuiombea nchi amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alisema, maendeleo yanayoendelea kupatikana hadi hivi sasa yametokana na matunda ya kuwepo kwa amani hapa Nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa kuirudisha amani inapopotea ni jambo gumu ikilinganishwa na urahisi wa kuitunza na kusema kuwa kuna mifano halisi ya mataifa yanayoendelea kukumbwa na migogoro mikubwa kutokana na kuvunjika kwa amani.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwaasa waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wote kwa ujumla kuendeleza moyo wa mshikamano na kudumisha amani kama msingi wa kila hatua ya maendeleo ya taifa.