RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahimiza wawekezaji wazalendo kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya utalii hapa nchini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo baada ya kuifungua rasmi hoteli ya Zanbreeze Beach Resort and Spa iliyopo Kikungwi, Mkoa wa Kusini Unguja leo, Agosti 16, 2025.
Amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ni juhudi za pamoja kati ya Serikali na wawekezaji wazawa katika kukuza uchumi na kuzalisha ajira kwa vijana, na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mazingira rafiki ili waweze kushindana na wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Ameeleza kuwa sekta ya utalii imepata mafanikio makubwa kutokana na ongezeko la wageni wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali nchini, ambapo jumla ya miradi 202 yenye thamani ya dola za Marekani Bilioni 2 imesajiliwa na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji (ZIPA).
Miradi hiyo imechangia ongezeko la wageni kutoka 260,000 mwaka 2020 hadi 736,000 mwaka 2024, huku Mkoa wa Kusini ukiongoza kwa kusajili miradi ya hoteli, ambapo kati ya miradi 202, miradi 105 ipo katika mkoa huo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali imeimarisha Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar kuwa kituo kimoja cha huduma kwa wawekezaji, ambapo huduma za usajili sasa zinapatikana kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na mwekezaji anaweza kupata cheti cha uwekezaji ndani ya saa 24 endapo atakamilisha taratibu zinazohitajika.
Halikadhalika, alisema Serikali imepitisha sheria mpya ya mwaka 2023 inayolenga kuwalinda wawekezaji wazalendo, ili waweze kuwekeza kwa mitaji midogo katika sekta ya utalii, kumudu vigezo vya uwekezaji na kunufaika na fursa zilizopo.
Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa ongezeko la watalii wanaokuja nchini linaakisi ukuaji wa uchumi na ongezeko la mapato ya kodi katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande mwingine, amewataka wawekezaji na wananchi kuendeleza utalii unaozingatia utunzaji wa mazingira katika miradi mikubwa ya uwekezaji kwa ajili ya manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.