RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa sekta ya Uhandisi na Usanifu wa Majengo ni kiungo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya miundombinu, ustawi wa jamii, na ukuaji wa uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua Semina ya Wataalamu wa Usanifu wa Majengo wa Afrika Mashariki inayofanyika katika Hoteli ya Madinat Al Bahr, Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi Julai 10, 2025.
Ameeleza kuwa taaluma ya usanifu wa majengo ni nyenzo muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ongezeko la idadi ya watu mijini, pamoja na kuimarisha haiba na mpangilio wa miji.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa usanifu unaozingatia na kulinda urithi wa utamaduni wa Afrika Mashariki, akieleza kuwa ushirikiano wa pamoja na ushauri wa kitaalamu miongoni mwa nchi za ukanda huu ni jambo la msingi ili kunufaika ipasavyo na sekta ya usanifu wa majengo.
Halikadhalika, amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) pamoja na Serikali ya Muungano (SMT) zitaendelea kushirikisha taaluma ya usanifu wa majengo katika shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wahitimu kujiajiri, kutumia fursa zilizopo, kurejesha stadi za ujuzi na elimu kwa wanagenzi vyuoni, sambamba na kuandaa bajeti mahsusi za kufanikisha tafiti bunifu.
Rais Dkt.Mwinyi alisema, Tanzania ni nchi inayoendelea iliyofikia uchumi wa kati, hatua iliyochangiwa na kuwepo kwa miradi mikubwa ya kimkakati inayoongeza pato la taifa, na kujivunia kuwa na wataalamu weledi wazawa, wakiwemo washauri elekezi wenye uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi ya usanifu kwa ubora wa hali ya juu.
Amewahakikishia wataalamu hao kuwa Serikali itaendelea kuwashirikisha kikamilifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya kimkakati kwa kuzingatia dhana ya kuwajengea uwezo na kuwaamini wasanifu wazawa.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ametunukiwa tuzo maalum ya “Mjenzi Shujaa” na kupokea tuzo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.