RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, michezo ni nyenzo muhimu na alama ya kuwaunganisha watu wa jamii na Mataifa mbalimbali katika kuimarisha ushirikiano, upendo na umoja.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Disemba 24, 2025 alipolifungua rasmi Tamasha la Michezo la Afed Sports Festival Zanzibar 2025, linalofanyika katika Viwanja vya Maisara Sports Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ameeleza kuwa kufanyika kwa mashindano hayo hapa Zanzibar ni tukio la kihistoria na kumbukumbu muhimu kwa Jumuiya ya Khoja Shia Ithnashir, mashindano ambayo yalianzishwa miongo kadhaa iliyopita katika mataifa mbalimbali duniani.
Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inajivunia kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza, yakishirikisha wanamichezo wapatao 300 kutoka jumuiya mbalimbali za Khoja Shia Ithnashir duniani, wakiwemo wanaume na wanawake.
Ameeleza kuwa mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kuleta furaha, upendo, mshikamano na kukuza vipaji vya michezo.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa michezo, mbali na kuleta burudani, hufundisha nidhamu, heshima na udugu, na ni kichocheo cha ushirikiano miongoni mwa jamii.
Ameongeza kuwa ni fursa muhimu ya kukuza uchumi, biashara, sekta ya usafirishaji na kuibua fursa mbalimbali za ajira na uwekezaji kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo kuzingatia maadili ya upendo, uhusiano mwema na udugu ili kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa, sambamba na kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii na maeneo ya kihistoria ya Zanzibar.
Katika hatua nyingine, ameipongeza Taasisi ya Africa Sports Federation kwa kuandaa semina maalum ya wawekezaji itakayojadili fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo Zanzibar kwa wageni wanaoshiriki mashindano hayo kutoka Mataifa mbalimbali, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uchumi, maendeleo na ushirikiano wa kimataifa wa kiuchumi.
Awali, Katibu wa Jumuiya ya Islam Jammat ya Zanzibar, ambayo ndiyo mwenyeji wa mashindano hayo, Ndg. Hassan Mohamed Raza, amesema kufanyika kwa ma