RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quraan ni kielelezo thabiti cha kuwepo kwa Uhuru wa kuabudu hapa nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipozungumza katika Mashindano ya 25 ya Kimataifa ya Mabara yote katika Kuhifadhi Quraan yalioandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma Foundation yàliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewasihi wazazi kuwahimiza watoto wao Kuhifadhi Quran ili kuongeza Masheikh na Maulamaa wa baadae.
Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza waumini wa Dini ya Kiislamu kuisoma na kuhifadhi Quran Tukufu, hasa katika Mwezi huu wa Ramadhani, huku wakitubu na kusaidia jamii wenye uhitaji.
Aliyeibuka mshindi wa mashindano hayo ni Aimeddin Farkhudinov kutoka Urusi; nafasi ya pili imeshikwa na Abdulmuhaimin Jumah kutoka Libya, mshindi wa tatu akawa Eslam Ahmed kutoka Misri.
Washiriki wengine walioshiriki wametokea nchi mbalimbali duniani zikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya, Ivory Coast, Nigeria, Burundi, Rwanda, Namibia, Morocco, Australia, Uingereza na Marekani.