Rais Mwinyi: Kudumisha amani ni wajibu wa kila mwananchi

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa kudumisha amani ni jukumu la kila mwananchi anayependa maendeleo ya nchi.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, Oktoba 18, 2025, aliposhiriki Sala ya Ijumaa na Dua Maalum ya kuiombea nchi pamoja na Uchaguzi Mkuu, iliyofanyika katika Msikiti wa Muembe Shauri, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kuwa jukumu la kulinda na kudumisha amani si la mtu mmoja pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha utulivu unaendelea kuwepo katika nafasi yake.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya umoja na maendeleo katika sekta zote, hivyo jamii inapaswa kuendelea kuhubiri amani na utulivu, hasa katika kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne iliyopita yametokana na kuwepo kwa amani, hali iliyowezesha Serikali kutekeleza mipango yake kwa ufanisi.

Vilevile, amewakumbusha wananchi kuwa maneno au vitendo vya mtu vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani, hivyo kila mmoja anapaswa kuchunga kauli na matendo yake.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa vurugu katika nchi mara nyingi haziwezi kuanza kwa bunduki, bali kwa maneno au matendo madogo madogo ambayo baadaye husababisha migogoro na machafuko.

Amehimiza wananchi wote kuendeleza hali ya utulivu iliyopo sasa, kabla, wakati na baada ya uchaguzi, sambamba na kufuata maelekezo ya uchaguzi siku ya kupiga kura ili demokrasia ichukue nafasi yake ipasavyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here