RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kisera ili kuhakikisha Zanzibar inapata nishati ya umeme wa uhakika wakati wote.
Akizindua Sera ya Nishati ya Zanzibar ya 2025 pamoja na Mpango Mkuu wa Umeme wa Zanzibar wa 2025–2040, katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi alisema sekta ya nishati ndiyo uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Serikali ya Awamu ya Nane imelenga kujenga Zanzibar yenye uchumi shindani, kijani na jumuishi kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, nafuu na salama.
Rais Dkt. Mwinyi amesema sera hiyo inalenga kupunguza gharama, kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuboresha ufanisi na kupunguza utegemezi wa kuni na makaa, hususan kwa wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, Serikali inaendeleza mikakati ya kuwekeza katika vyanzo mbadala vya nishati ikiwemo jua, upepo, gesi asilia na mifumo ya akiba ya umeme (Battery Storage), sambamba na kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Rais Dkt. Mwinyi aliwapongeza watendaji wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini, wataalamu, Shirika la Umeme, Benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) kwa kushirikiana kufanikisha uandaaji wa sera hiyo muhimu.
Akizungumzia vitendo vya hujuma katika miundombinu ya umeme, Rais Dkt. Mwinyi alitoa agizo la kuchukuliwa hatua kali dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
