RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar inahitaji wawekezaji zaidi, hususan katika sekta ya utalii na uwekezaji, ambazo ni sekta za kipaumbele kwa ukuaji wa uchumi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai, aliyefika Ikulu Zanzibar leo Julai 22, 2025.
Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Canada kwa kuendelea kutoa misaada ya maendeleo kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar.
Ameeleza kuwa misaada ya nchi hiyo katika sekta ya elimu na afya imekuwa na mchango mkubwa katika kuleta mageuzi ya kimkakati ya kuimarisha huduma za afya na maendeleo ya elimu hapa nchini.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amemueleza Waziri Randeep kuwa bado zipo fursa nyingi zaidi za kuwekeza Zanzibar, huku akibainisha uwepo wa sera na vivutio maalum kwa wawekezaji wanaowekeza visiwani humo.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao, Dkt. Mwinyi ameihakikishia Canada kuwa uchaguzi huo utakuwa huru, wa amani na utulivu, kutokana na kuimarika kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliosaidia kuwaunganisha wananchi na kudumisha hali ya amani na utulivu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, hali ambayo anaamini itaendelea hata wakati na baada ya uchaguzi.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada, Randeep Sarai, ameihakikishia Zanzibar kuendelea kwa ushirikiano na utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo zinazofadhiliwa na nchi hiyo, hususan katika sekta za elimu na afya.