Rais Mwinyi aahidi kujenga uwanja kwa ajili ya AFCON 2027

0

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kujenga uwanja mkubwa wa soka kwa ajili ya michuano ya CAF ambao utakuwa zaidi ya Wembley na Old Trafford vya Uingereza.

Akizungumza wakati wa kuzindua viwanja vya michezo vya Maisara Complex, Dkt. Mwinyi alisema uwanja huo utajengwa kwa ajili ya Michuano ya Mataifa ya Africa (AFCON 2027).

“Kuna mtu aliuliza kuhusu AFCON, nani wale, eeeh Al-Jazeera, kuna kitu kitashuka hapa Zanzibar kitakuwa zaidi ya Old Traford, zaidi ya Wembley” alisema Dkt. Mwinyi.

Alisema, pia kutajengwa viwanja vingine kama hivyo vya Maisara katika wilaya na mikoa yote ya Zanzibar kinachotakiwa ni amani na utulivu ili malengo hayo yaweze kufikiwa.

Ujenzi wa viwanja hivyo vya Maisara ambako kuna viwanja vya michezo mchanganyiko ni sehemu ya ahadi na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, ikiwa ni pamoja na viwili vya tenisi.

Viwanja vingine ni viwili vya mchezo wa Padel na vingine vya idadi hiyo vya soka, na vinne vya michezo mchanganyiko ambayo ni kikapu, mpira wa mikono, netiboli na wavu.

Dkt. Mwinyi ameagiza Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi na uendeshaji wa viwanja hivyo ili viweze kubaki katika ubora wake.

“Tunataka tukirudi baada ya miaka mitano tuvikute kama vilivyo leo,” alisema Rais Dkt. Mwinyi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here