Rais Dkt. Mwinyi asisitiza uzalendo na uwazi katika utumishi wa umma

0

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza Watumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa uzalendo, uwajibikaji na uadilifu, kwa kuzingatia misingi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ili kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Amesema kuwa lengo kuu la Serikali ni kuimarisha maslahi ya Watumishi wa Umma kulingana na ukuaji wa uchumi wa nchi, ambapo Serikali imepanga kufikia ukuaji wa asilimia 10 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 7.4.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 25, 2025, katika hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, iliyofanyika katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya Utumishi wa Umma, ikiwemo kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza mishahara, posho, na pensheni kwa wastaafu, hatua inayoakisi dhamira ya Serikali ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma, kuongeza uwazi na kupunguza urasimu katika taasisi za umma.

Amefafanua kuwa mifumo kama Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Malipo (HCMIS) imeleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa rasilimali watu na malipo ya watumishi, na amewataka watumishi kuipokea na kuitumia ipasavyo ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeweka mifumo inayozingatia kiwango cha elimu, uzoefu na muda wa ajira, hatua ambayo imechangia kuongeza ari na motisha kwa watumishi wa umma.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya watumishi, ambapo watumishi 1,519 wamepata mafunzo ya muda mrefu ndani ya nchi, 65 nje ya nchi, na wengine 631 wamepata mafunzo ya muda mfupi nje ya nchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema lengo la Serikali ni kuwa na kizazi kipya cha Watumishi wa Umma wenye maarifa, ujuzi na mitazamo mipya inayolenga kuimarisha utumishi na kuleta maendeleo endelevu ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here