Na Mwandishi Wetu, Pemba
KADA wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF), Ali Abdallah Ali maarufu kwa jina la Swedi Abdallah Ali, amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (SMZ), Dkt. Hussein Ali Mwinyi ndiye mtu ambaye amemfanya aachane na chama chake cha zamani na kujiunga tena na CCM.
Akizungumza na wanahabari katika bandari ndogo ya Shumba Mjini, iliyopo wilaya ya Micheweni, Pemba alisema, maendeleo aliyoyaleta ndani ya kipindi kifupi ndio yaliyomfanya arejee tena katika chama chake hicho.
“Awali nilikuwa TANU na baadae CCM, lakini baada ya kifo cha Karume niliachana na chama hicho…nasema Mungu azidi kumjaalia ya heri (Dkt. Mwinyi) na kama ikiwezekana abakie madarakani hadi atakapotaka mwenyewe,” alisema.
Alibainisha kuwa, Rais Dkt. Mwinyi amefanya mambo makubwa ambayo amemzidi hata Rais wa kwanza, Abeid Karume ambaye nae alikuwa na nia ya dhati ya kubadili maisha ya waZanzibar.
“Hakika tushukuru Mungu kutupatia mtu mwenye maono na mapenzi kwa binadamu wenzake na Inshallah Mwenyezi Mungu atakuwa nae daima” alisema na kuongeza kuwa watu wanataka maendeleo na sio porojo zisizo na maana.
Alisema, bandari hiyo itakuwa kituo muhimu cha biashara na Mji wa Mombasa nchini Kenya ambao upo maili chache kutoka Shumba mjini na pia itasaidia mwingilio usio rasmi uliokuwa unafanywa wakatIi huo ilipokuwa bandari bubu.