Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MWENYEKITI wa ACT Wazalendo ambaye pia ametangaza nia ya kuwania Urais Zanzibar, Othman Masoud Othman ‘OMO’, anatajwa kuwa ni mtu hatari na hafai kuwa kiongozi.
Kauli hiyo ya CCM ambayo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis wakati wa mkutano na wanahabari, Mjini Zanzibar.
Mbeto akiwa na ushahidi wa video mbili tofauti zinazomuonyesha Mwenyekiti huyo akitoa kauli zinazopingana katika jambo moja, alisema zinabainisha jinsi gani ilivyo hatari kumpa dhamana ya uongozi mtu wa namna hiyo.
Katika mkutano na wanahabari mara baada ya kujiandikisha kama mpiga kura mpya katika kituo cha Mpende, Mwenyekiti huyo alisema anajiandikisha upya kutokana na kutowepo nchini 2020.
“Mimi ni mpiga kura toka mwaka 1990 na sijawahi kukosa kupiga kura, lakini bahati mbaya 2020 nilikuwa na kazi za watu nje ya nchi hivyo wakati wa kurekebisha taarifa kwenye daftari sikuwepo” alisema.
Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida Mwenyekikti huyo akiwa katika mkutano wa hadhara wa chama chake cha ACT Wazalendo, eneo la Nungwi, Kaskazini Unguja, anatoa madai mapya.
Mwenyekiti huyo anadai kuwa 2020 kuna watu 82,000 walitolewa kwenye daftari la wapiga kura na yeye ni mmojawapo.
“Kuna watu 82,000 walitolewa kwenye daftari 2020 kinyume na utaratibu na sheria ya uchaguzi inavyosema,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alibainisha kuwa walitolewa kinyume cha sheria na utaratibu wa tume ya uchaguzi na sheria iliyotumika sio sawa na ndio maana akaenda kujiandikisha upya.
Mwenezi Mbeto wa CCM, alisema katika mkutano huo kuwa ni aibu kwa kiongozi mkubwa kama huyo anayetarajia kuwania Urais kusema uongo tena hadharani.
“Niliwahi kusema awali kuwa Othman Masoud Othman hajawahi kuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema Mbeto na kuongeza kuwa kauli zake zinaonyesha asivyo mkweli.
Mbeto alibainisha kuwa Mwenyekiti huyo wa ACT Wazalendo hajawahi kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Mwenezi Mbeto alibainisha kuwa Othman Masoud Othman 1990 alikuwa mwanasheria mkuu wa Serikali atuambie kura alipiga kituo gani.
“Unapoenda kubadilisha taarifa zako kwenye daftari unaenda na kitambulisho chako cha kupigia kura lakini yeye hakuwa nacho”
Mbeto alisema sifa mojawapo unayotakiwa kuwa nayo unayeenda kuandikishwa ni kuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkazi ambacho alienda nacho kwenye kujiandikisha.
“Kama 2020 hakuwepo nchini na anajinasibu kuwa ni mpiga kura toka 1990 basi aonyeshe kitambulisho kupigia kura cha zamani,” alisema Mwenezi huyo.
Mbeto alibainisha kuwa hata katika Hifadhi Data ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inaonyesha Othman Masoud Othman ni mpiga kura mpya aliyejiandikisha mwaka huu katika kituo cha Mpendae.
Alisema, madai kuwa eti jina lake na wengine 82,000 lilitolewa kwenye daftari ni uongo ambao haukupaswa kutolewa na mtu wa aina yake.
Alisema, kulingana na sheria za uchaguzi, wenye sifa ya kutolewa kwenye daftari ni waliofariki na ambao wameenda wenyewe kurekebisha taarifa zao.
“Sasa yeye anasema alikuwa nje 2020 sasa alijuaje kuwa katolewa wakati hata kituoni hakwenda” alisema Mbeto.
Alisema, yawezekana mtu anahama kikazi au anahamisha makazi linapoletwa daftari kwa ajili ya uhakiki na kujiandikisha ndio anaenda kurekebisha taarifa zake.
“Ebu mwambieni awaonyeshe kitambulisho chake cha zamani cha mpiga kura” alisema na kubainisha kuwa OMO, hajawahi kumpigia kura marehemu Maalim Seif wala waliowahi kumteua kushika nafasi mbalimbali Serikalini.
Mbeto alisema, kuna maofisa wengine wana nyadhifa kubwa serikalini na hawajahi kupiga kura lakini hawawadanganyi wananchi.
“Kiongozi huyo anapaswa kuwa mkweli kwa wananchi wa Zanzibar, alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, atuambie taarifa zake zipo kituo kipi?” anahoji Mbeto.
Alisema, sheria inataka ukienda kurekebisha taarifa lazima uwe na kitambulisho chako, lakini yeye hana ndio maana changu ninacho hiki hapa yeye cha kwake kipo wapi?
Mbeto alisema, hata kujikiandikisha ndio maana ameenda Mpendae na sio nyumbani kwake Mbweni kwani hakuwa na sifa.
“Hata huku Mpendae sifa ya kukaa miezi 36 ipo kimchongo tu kwani hata mtaa anaokaa alisaidiwa kutajiwa, haujui,” alisema mwenezi Mbeto.
Alitoa angalizo kwa Wanzanzibar kuwa makini na watu aina ya OMO ambao ni watafuta madaraka wasio na uzalendo kwa nchi n ahata ACT Wazalendo wanajua wamekosea kumpa madaraka kwenye chama mtu kama OMO.