Ofisi ya Msajili wa Hazina, WCF na PSSF waingia ubia kumiliki kiwanda cha Mponde

0

OFISI ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), pamoja na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), wameingia ubia wa kumiliki Kiwanda Cha Chai cha Mponde kwaajili ya kuongeza tija katika uzalishaji, huku wadau mbalimbali wakitakiwa kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika zao la Chai.

Katika ubia huo Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa niaba Serikali inamiliki hisa ya asilimia 16, huku PSSSF na WCF wanamiliki asilimia 42 kila mmoja jambo ambalo litaongeza kasi ya utendaji katika ushindani wa soko na kuifanya Taifa kupata gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine.

Akizungumza jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya kumiliki kiwanda hicho iliyofanyika katika Ofisi ya PSSSF, Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu, alisema uwekezaji huo unakwenda kuongezeka thamani ya kiwanda kutoka Shilingi Milioni 790 zilizopo na kufikia Bilioni 4.8.

Mchechu alisema, wanatarajia kuwekeza Shilingi Bilioni nne ambapo mpaka sasa tayari uwekezaji katika kiwanda hicho umefika Bilioni 2.5.

“Kiwanda hiki kinakwenda kufufua uchumi kwa wakazi wa Korogwe na wakulima wa zao la chai watapata fursa ya kupata soko la uhakika wa kuuza mazao yao” alisema Mchechu.

Mchechu aliongeza, kupitia uwekezaji huo, Serikali inakwenda kunufaika na ulipaji wa kodi, huku akisisitiza umuhimu wa Menejimenti kuongeza ufanisi katika utendaji ili waweze kuleta gawio kama ilivyo kwa taasisi nyingine.

“Nawashukuru sana PSSSF, WCF kwa kukubali wito wa kwenda kufanya uwekezaji katika sekta ya kilimo cha chai, ukiangalia tuna ardhi nzuri ambayo tunaweza kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali nchini” alisema Mchechu.

Aidha, alisema Tanzania kuna ardhi kubwa na yenye rutuba ambayo inakubali kilimo cha chai hasa Mikoa ya Iringa na Mbeya, huku akieleza kuwa kulikosekana wawekezaji wa viwanda katika zao la chai ambalo linalimwa kwa muda mrefu na kuleta tija.

“PSSSF na WCF wanapoonekana katika uwekezaji sekta ya kilimo itawavutia wadau wengine na kufanya vizuri sekta hii, kwani kwa muda mrefu wakulima walishindwa kulima zao la chai kutokana na kukosa soko la uhakika” alisema Mchechu.

Mchechu amebainisha kuwa Tanzania inazalisha kiwango kidogo cha chai na kufanya mauzo kuwa dola milioni 50 kwa mwaka, tofauti na nchi jirani ya Kenya ambao wanauza zaidi ya dola Bilioni moja.

“Tupo chini katika mauzo kwa sababu tuna mwamko mdogo wa kufanya uwekezaji katika zao la chai, lakini leo tunashukuru tunawapa nafasi kiwanda hiki, menejimenti, bodi kuanza kukimbia katika utekelezaji wa majukumu yao” alisema Mchechu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma amesema kuwa uwekezaji huo unakwenda kuibua uchumi wa wananchi katika mkoa husika, kwani wakulima wengi wa eneo wanakwenda kuuza zao la chai katika kiwanda hicho.

“Ni busara imetumika kutumia fedha za Mifuko kuleta hapa kwa ajili ya kufanya uwekezaji na kuleta faida kwa kiwanda na Wananchi” alisema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF Bw. Abdul -Razaq Badru alisema, uwekezaji huo ni sehemu ya mipango yao kutimiza jukumu linalotarajiwa na Serikali kuwekeza katika maeneo yenye mchango kwa wananchi na wanachama wao.

“Tumefarijika kuwekeza katika sekta ya kilimo sehemu ambayo inatoa mchango mkubwa kwa Taifa, tutaendelea kushiriki katika maeneo mengine na kuleta tija kwa wananchi” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here