Ni vema tukajipanga na kuanza upya kuijenga Taifa Stars

0

Na Yahya Msangi

Kuna nchi zimefanikiwa kuondokana na maudhi kwa kutambua haraka kuwa mpira umewashinda, baada ya kutambua udhaifu wao wakatafuta tiba. Kila mmoja akatafuta tiba inayomfaa na wamefanikiwa.

Mathalani Marekani ya Kaskazini wao wakaamua kuachana na mpira wa miguu na kuwekeza zaidi kwenye ngumi, mbio, mpira wa vikapu, ‘Baseball’ na ‘American Football’. Wakafanikiwa haswa. Kuna miaka hawakujishughulisha kabisa na Michuano ya Kombe la Dunia, walijua hata wakishiriki hakuna watakachoambulia.

Kuna nchi Ulaya ziliamua kuwa mpira hawauwezi mfano ni Iceland, Finland, Luxembourg na nyinginezo, wakaamua kuwekeza kwenye michezo ya kwenye barafu. Ireland wao wakawekeza kwenye raga.

Barani Afrika kuna nchi ziliamua kuvunja mashirikisho yao ya soka na kujitoa mashindano ya CAF na FIFA licha ya faini zilizokuwepo. Ghana ni moja ya nchi hizo, wakajiandaa vyema na kurudi kwa kasi, nguvu na ari mpya.

Nchi nyingine ni India na Pakistan. Wao walipojitambua hawawezi mpira, wakajikita kwenye Kriketi, huko wao ndio wababe wa dunia, hata Ufaransa kuna wakati walijipima wakaona hawana wanachofanya kwenye soka, wakaweka nguvu kubwa kwenye raga. Ni sawa na Australia, New Zealand, Tonga, Samoa na wenzao wa visiwa vya Pasifiki.

Sisi licha ya kuendelea kuboronga kila kukicha na kuwaudhi mashabiki wa soka na watanzania kwa ujumla, bado tunaendelea kushiriki michuano mbalimbali na kuambulia patupu, ni kwasababu tumekataa kuukubali ukweli. Matokeo ni huzuni ya kujitakia kila mwaka. Yaani toka 1974 ni majonzi! Ni kwa kuwa kichwa cha mwendawazimu kimeukataa ukweli.

Imefika mahali ni lazima kwanza tuukubali ukweli. Mpira umetushinda! Tukiukubali ukweli huu, tutaacha kusajili wachezaji kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Togo, Zambia, tutaacha kushabikia Yanga na Simba na kujidanganya tunaujua mpira.

Tutaacha kuchagua viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kuangalia ushabiki wao wa Simba na Yanga. Tutaacha kuajiri makocha wasio na sifa. Tutaacha kung’oa viti vya uwanja wa kisasa wa Taifa.

Hapo, tutakaa chini na kujiuliza tuachane na soka tuwekeze kwenye ngumi au kwenye mieleka, kulenga shabaha, riadha au kwenye mashindano ya kunywa mbege na pombe? Au tukiamua tuendelee na soka tuamue kujitoa kwa miaka hata mitano kushiriki mashindano yote hata kama tutalazimika kulipa faini.

Tukijitoa, tujiulize tufanye nini kabla ya kurejea? Serikali ibebe majukumu gani? TFF iweje? Wachezaji walelewe na wapatikane vipi? Je, tuvunje Yanga na Simba maana nazo zinachangia kuua soka nchini? Watanzania wamechoka maumivu haya ya kila siku, wanataka kuona timu yao ikifika mbali na kufanya vizuri. Ni vema tukajipanga na kuanza upya!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here