WASHNGTON, Marekani
KUNA uwezekano wa Hillary Clinton akajitosa kugombea kwa mara ya tatu katika uchaguzi wa urais wa Marekani unaotarajia kufanyika 2024.
Hillary Clinton, ambaye alikuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuwa mpinzani wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, katika uchaguzi wa 2016, amenukuliwa akitoa kauli zinazoonyesha anajipanga kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Akizungumzia suala hilo, msaidizi wa zamani wa Bill Clinton, Dick Morris, alisema katika mahojiano ya redio kuhusu uwezekano wa Hillary Clinton kugombea tena kwamba “anajiandaa kuingia katika uchaguzi wa 2024 kama chaguo la wastani kwa Wanademokrasia.”
Akiashiria kauli za hivi karibuni za Hillary Clinton kwamba Wamarekani hawaamini mipaka iliyo wazi, “Kila siku kunajitokeza dalili zaidi za uamuzi wa Hillary kushiriki katika uchaguzi ujao wa urais kama mgombea wa wastani.”
Msaidizi huyo wa zamani wa Bill Clinton alisema, kuna uwezekano wa chama cha Democrats kumpitisha Hillary Clinton kuliko Rais wa sasa wa Marekani, Joe Biden, kwa sababu ya hofu ya kushindwa.
“Wademokrati wanaona kuwa, uwezekano wa kushinda mgombea mwenye misimamo ya wastani ni mkubwa zaidi katika uchaguzi ujao,” aliongeza.
Akinukuliwa na ‘Financial Times,’ Hillary Clinton alisema, Marekani iko kwenye ukingo wa kupoteza demokrasia, na suala hilo litakuwa hatari zaidi katika uchaguzi wa urais wa 2024 kwa kutilia maanani wagombea waliopo sasa.