Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka Mfuko amesema, mfuko huo umeimarisha kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kifedha na kufikisha bakaa ya Shilingi Trilioni 1.31 hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26, rasilimali zinazouwezesha kuhimili majukumu yake kwa zaidi ya miaka miwili.
Dkt. Irene alisema hayo kwenye kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), na kuweka wazi kwamba, hali hiyo inawawezesha kufanikisha ulipaji wa madai ya watoa huduma, utimizaji wa mahitaji ya Wanachama, na weledi katika kukabiliana na mabadiliko ya huduma za afya.
Alisema, muda wa wastani wa kulipa madai ya watoa huduma umepungua kutoka siku 120 hadi 50, chini ya ukomo wa siku 60 unaotajwa kisheria. Pia, wanachama wakuu wameongezeka kwa asilimia 17, wategemezi kwa asilimia 6.2, huku mtandao wa vituo vinavyoshirikiana na NHIF ukifikia zaidi ya 10,300.
“Pamoja na mafanikio haya, kadiri wigo wa wanufaika unavyozidi kupanuka, Mfuko utaendelea kuimarisha tathmini ya vihatarishi, usimamizi wa madai, na upangaji madhubuti wa rasilimali ili kudumisha uhimilivu na uendelevu wake wa kifedha kwa siku za usoni,” alisema Dkt. Irene.
Aidha, alisema Mfuko umeendelea kubuni bidhaa jumuishi za bima ya afya zinazolenga wananchi wenye uwezo na mahitaji tofauti ya kiuchumi. “Kupitia kifurushi cha makundi, wananchi wanaweza kujiunga wakiwa katika vikundi vya kuanzia wanachama 10 kwa mchango wa Shilingi 60,000 kwa mwaka kwa kila mwanachama.”
Alisema, mpango huu unawalenga wananchi wa sekta isiyo rasmi wakiwemo wakulima, wavuvi, wafanyabiashara wadogo, waendesha bodaboda, na mama lishe ili kupunguza changamoto za gharama za kujiunga mmoja mmoja; hivyo, wananchi wanahimizwa kutembelea ofisi za NHIF kupata maelezo zaidi na kujiunga kupitia vikundi vyao.
Mbali na ubunifu huo, alisema Mfuko unaendelea kutoa elimu thabiti kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mikutano ya hadhara, maonesho, majukwaa ya kidijitali, na ushirikiano na viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na wadau, ili kutoa ufahamu kuhusu umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua, bidhaa zinazopatikana, na taratibu za kupata huduma.
“Lengo kuu likiwa ni kujenga uelewa kwa jamii kuwa bima ya afya ni mfumo madhubuti wa kujikinga na gharama za matibabu mapema, badala ya kuwa suluhisho la dharura wakati ugonjwa umeshajitokeza,” alisema Mkurugenzi huyo wa NHIF.