MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga amesema fedha za michango ya wanachama wa mfuko huo zipo salama na kwamba, taarifa zinazodai fedha hizo zimeliwa ni upotoshaji.
Konga alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada mbele ya Wahariri na Waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya Mfuko huo kwa kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.
Alisema, NHIF hawajagawana fedha za wanachama kama inavyodaiwa, badala yake wametoa mikopo kwa watoa huduma na watumishi kwa kufuata taratibu ili wanachama na wananchi wapate huduma nzuri, na wanufaika wanarejesha mikopo hiyo.
“Fedha za wanachama zipo salama, hatugawana, mengi yanayosemwa ni upotoshaji, vyombo vya Serikali vimechunguza na vimegundua hakuna tatizo, hivyo nawasihi wanachama wetu wasiwe na hofu,” alisema Konga.
Akifafanua kuhusu mikopo hiyo Konga alisema, ipo ya aina mbili; mkopo wa kwanza wanawapa watoa huduma kwa ajili ya kuboresha majengo kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya, kununulia vifaa tiba na kuimarisha mfumo wa TEHAMA.
Mkopo wa pili unatolewa kwa watumishi wa sekta ya afya kwa ajili ya kuwawezesha kukidhi mahitaji yao ikiwemo kujiendeleza kielimu, kujenga nyumba na matumizi mengine ambayo wanaona yatawafanya watimize majukumu yao bila changamoto.
Aidha alisema, watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha michango ya wanachama inatumika vizuri, na hawapo tayari NHIF igeuzwe kuwa shamba la bibi “tutakuwa wakali na tutachukua hatua kwa watakaokiuka taratibu na kuhatarisha uhai wa Mfuko.”
Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, alisema Mfuko umeendelea kusajili wanachama wachangiaji, pia wameongeza idadi ya vituo. “hadi kufikia Desemba 2023, NHIF ilikuwa na jumla ya vituo 9,467 vilivyosajiliwa ili kutoa huduma kwa wanachama wake.”
Konga alisema, kati ya vituo hivyo 6,852 sawa na asilimia 72 ni vya Serikali huku vituo binafsi vikiwa ni 1,766 sawa na asilimia 19.
Mbali na mafanikio hayo, alisema wamefanikiwa kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utambuzi, usajili wa wanachama, ukusanyaji wa michango, uwasilishaji, uchakataji na ulipaji wa madai na kusisitiza kuwa “Uwekezaji kwenye TEHAMA haukwepeki,”
Alisema, wameanzisha Mfumo wa wanachama kujisajili, kupata namba ya malipo n.k kwa kutumia mfumo wa Kielektroniki (USSD Code 15200#) na mtandao, jambo ambalo linamfanya mwananchi kukamilisha taratibu za kuwa mwanachama bila kufika kwenye ofisi zao.
Mkurugenzi huyo aliendelea kusema, wameboresha muundo wa Mfuko ili kukidhi mahitaji ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. “Uhalisia unaonesha kuwa asilimia 85 ya Wananchi hawana Bima ya Afya na hivyo kukosa uhakika wa huduma bora za afya kipindi wanahitaji.”
Konga alisema, sababu ya kuandaliwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kutimiza wajibu wa Serikali wa kikatiba wa kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila vikwazo.
Mbali na hayo pia wameongeza wigo wa mtandao wa vituo vya kutolea huduma za afya kwa kushirikisha wadau mbalimbali nchini huku wakihakikisha wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa wanazipata kwa urahisi.
Alisema, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu na wataalamu katika sekta ya afya nchini, wagonjwa wa saratani na figo wanapata huduma karibu na maeneo walipo kwa kutumia huduma za NHIF.
“Gharama za kugharamia wagonjwa wa saratani kwa mwaka 2023/2023 zilikuwa Shilingi Bilioni 32.46, ukilinganisha na Shilingi Bilioni 12.25 mwaka 2021/2022. Gharama za matibabu ya figo zilikuwa Shilingi Bilioni 35.40 na Shilingi Bilioni 11.45”, alisema.
Alisema, wameimarisha utambuzi wa wanufaika vituoni ili kuepuka udanganyifu wa kadi moja kutumiwa na mtu zaidi ya mmoja ambapo wameweka watumishi wao kwenye vituo vyote kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.
“Haiwezekani kadi moja ya Shilingi 50400 ihudumie watoto wanne, tumeweka watu wetu kwenye vituo ili kudhibiti udanganyifu na tukibaini tunachukua hatua kali,” alisisitiza Konga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Thobias Makoba alisema, Sekta ya Afya imekuwa ni sekta muhimu tangu Uhuru.
“Kati ya mashirika ambayo yanatusaidia kuepukana, kupiga vita maradhi na kutusaidia kuchochea maendeleo ni shirika (Mfuko) la NHIF,” alisema Makoba.
Aliongeza kuwa, katika Sekta ya Afya, NHIF ni moja wapo ya mashirika ya kimkakati katika maendeleo ya Tanzania, kwa sababu huduma wanazozitoa zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania.